• HABARI MPYA

    Monday, October 23, 2017

    LIGI YA WANAWAKE KUANZA NOVEMBA 26 DAR NA ARUSHA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LIGI ya Taifa ya Wanawake inayodhaminiwa na Azam TV, inatarajiwa kuanza Novemba 26, mwaka huu ikishirikisha timu 12 zitakazogawanywa katika makundi mawili.
    Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba kila kundi litakuwa na timu sita zikiwemo mbili zilizopanda msimu huu, Simba Queens na Alliance Academy baada ya kushuka kwa Viva Queens ya Mtwara na Victoria Queens ya Kagera.
    Madadi amesema kwamba Kundi A litakalotumia kituo cha Dar es Salaam litaundwa na timu za Mlandizi Queens ya Pwani, JKT Queens ya Kinondoni, Evegreen ya Temeke, Mburahati Queens, Simba Queens za Ilala na Fair Play ya Tanga.
    Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi amesema Ligi ya Taifa ya Wanawake itaanza Novemba 26, mwaka huu

    Kundi B Madadi amesema litakuwa na timu za Panama ya Iringa, Marsh Academy, Alliance za Mwanza, Kigoma Sisterz ya Kigoma, Bao Bab ya Dodoma na Majengo Queens ya Singida.
    Amesema hatua ya kwanza itafikia tamati Desemba 9 na kila kundi litatoa timu nne ambazo zitafuzu hatua ya pili ya ligi hiyo, itakayojulikana kama Super 8, itakayonza Desemba 20 hadi Machi 28, mwakani.
    Lakini kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, Madadi amesema kwamba kuna matukio yatatangulia, ikiwemo semina ya viongozi klabu na makamisaa ambayo itafanyika siku moja kabla ya kuanza kwa hatua ya makundi.
    Kuhusu usajili, Madadi amesema utaanza Oktoba 25 hadi  Novemba 10, wakati pingamizi dhidi ya wachezaji waliosajiliwa kimakosa zitawasilishwa kuanzia Novemba 12 hadi 17 na kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kitafuatia Novemba 18, kabla ya klabu kukabidhiw3a leseni za wachezaji Novemba 20.
    Bingwa mtetezi wa Ligi ya Taifa ya Wanawake ni Mlandizi Queens, ambayo ilibeba taji hilo Machi mwaka huu katika michuano iliyofanyika kwa mara ya kwanza Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIGI YA WANAWAKE KUANZA NOVEMBA 26 DAR NA ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top