• HABARI MPYA

  Saturday, August 05, 2017

  YANGA SC YAIZIMA SINGIDA UNITED 3-2...MARTIN SHUJAA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imetoka nyuma na kushinda mabao 3-2 dhidi ya Singida United katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Shujaa wa Yanga katika mchezo wa leo alikuwa ni kiungo mshambuliaji, Emmanuel Martin aliyefunga bao la ushindi kwa shuti la umbali wa mita 23 baada ya pasi ya mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.
  Singida walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa 2-1, mabao yote matatu yakifungwa na wachezaji wa kigeni kipindi cha kwanza.
  Kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tano kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib kuangushwa umbali wa mita 25.
  Kiungo wa Yanga, Emmanuel Martin akikimbia kushangilia baada ya kufunga bao la ushindi
  Mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma akiwatoka mabeki wa Singida
  Kiungo wa Singida, Mudathir Yahya akimlamba chenga kiungo wa Yanga, Raphael Daudi
  Beki wa Yanga, Kevin Yondan akiutelezea mpira miguuni mwa kiungo wa Singida, Kiggi Makasi 
  Mshambuliaji mpya wa Yanga, Ibrahim Hajib akipiga hesabu za kuwatoka wachezaji wa Singida

  Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda kwa misimu yote miwili iliyopita, Dany Usengimana akaifungia Singida United bao la kusawazisha dakika ya nane akitumia vizuri makosa ya nabeki wa Yanga kuchanganyana.
  Mshambuliaji Mzimbabwe, Simbarashe ‘Simba’ Nhivi Sithole akaifungia bao la pili Singida dakika ya 23 akitumia tena makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga.
  Kipindi cha pili, kocha Mzambia wa Yanga alibadilisha karibu kikosi kizima akimtoa hadi kipa Beno Kakolanya na kumuingiza Mcameroon, Yoouth Rostand.
  Mabadliko hayo yaliisaidia Yanga kupata mabao mawili dakika za mwishoni, akianza Mrundi Tambwe kusawazisha kwa penalti dakika ya 83 baada ya kipa Said Lubawa kumchezea rafu kiungo chipukizi, Said Juma, kabla ya Martin kufunga la ushindi dakika yab 90 na ushei.   
  Katika mchezo huo, Singida walipoteza mikwaju miwili ya penalti, wa kwanza dakika ya kwanza kabisa Elisha Muroiwa akipaisha juu ya lango na ya pili, kipa Rostand akiokoa shuti la pembeni la mshambuliaji Atupele Green.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Beno Kakolanya/Youth Rostand, Juma Abdul, Hajji Mwinyi/Hassan Kessy, Kevin Yondan/Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Abdallah Hajji ‘Ninja’, Thabani Kamusoko, Pius Buswita/Emmanuel Martin, Raphael Daudi/Juma Mahadhi, Donald Ngoma/Amiss Tambwe, Ibrahim Hajib/Said Juma na Baruan Akilimali.
  Singida United; Said Lubawa, Michael Rusheshagonga, Shafiq Batambuze, Elisha Muroiwa, Juma Kennedy, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Tafadzwa Kutinyu, Nhivi Simbarashe, Danny Usengimana na Kigi Makasi. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAIZIMA SINGIDA UNITED 3-2...MARTIN SHUJAA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top