• HABARI MPYA

    Sunday, August 13, 2017

    KARIA, WAMBURA SI WATU WAPYA KATIKA SOKA YA TANZANIA

    SOKA ya Tanzania jana imeingia rasmi katika zama mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika kwenye kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la St. Gasper mjini Dodoma kuuweka madarakani uongozi mpya.
    Hiyo ni baada ya Wallace Karia kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ushindi wa kishindo.
    Karia amewashinda mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Ally Mayay, Katibu wa zamani wa shirikisho hilo, Frederick Mwakalebela, Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Wakili Imani Madega, Mwandishi wa Habari za Michezo wa zamani, Shija Richard na Katibu wa klabu ya Mbeya City, Emmanuel Kimbe.
    Michael Richard Wambura ameshinda nafasi ya Umakamu wa Rais kwa kishindo pia, akiwaangusha Mwenyekiti wa FA ya Dodoma, Mulamu Nghambi, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
    Karia amepata kura 95 kati ya 125 zilizopigwa, akifuatiwa na Mayay na Shija  waliopata kura 9 kila mmoja,  huku Wambura akipata kura 85 kati ya 125, akifuatiwa na Mulamu Nghambi aliyepata kura 25.
    Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Lameck Nyambaya kutoka Kanda ya Dar es Salaam aliyepata kura 41, akifuatiwa na Shaffi Dauda aliyepata kura 21, Khaled Mohammed kwa Kanda ya Kilimanjaro na Tanga aliyepata kura 70 na Fransis Ndulami kura 7O Kanda ya Pwani na Morogoro.
    Wengine ni Mohamed Ally 35 kanda ya Dodoma na Singida, Dunstan Ditopile kura 74 Kanda ya Lindi na Mtwara, James Mhagama kura 63 Njombe na Ruvuma, Elius Mwanjala kura 61 Mbeya na Ruvuma, Kenneth Pesambili 72 Katavi na Rukwa, Issa Bukuku kura 80 Kigoma na Tabora, Sara Chau kura 57 Manyara na Arusha, Mbasha Matutu kura 67 Shinyanga na Simiyu, Modestus  Lufanga kura 67 Mara na Mwanza, Salim Chama kura 92 Kagera na Geita.
    Baada ya matokeo hayo, washindi wote waliapishwa kwa agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
    Ikumbukwe aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameshindwa kurudi kutetea nafasi yake baada ya kuwekwa rumande tangu Juni 29, mwaka huu kwa pamoja na Katibu weke, Selestine Mwesigwa na Mhasibu Isinde Isawafo Mwanga kwa tuhuma za ubadhirifu.
    Watatu hao walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
    Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani, lakini baada ya kesi hiyo kuanza kuunguurma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo ambaye sasa anakuwa Rais kamili.
    Hizi ni zama mpya kiutawala katika soka ya Tanzania – lakini sote tunafahamu Karia na Wambura si watu wapya ndani ya TFF, bali ni wapya katika nafasi zao za sasa tu.
    Wambura amewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF tangu inaitwa FAT (Shirikisho la Soka Tanzania) na katika kipindi chote hicho, Karia naye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, baadaye Makamu wa Pili wa Rais akiwakilisha klabu kabla ya kuwa Makamu wa Rais katika utawala uliopita.
    Hii inamaanisha watu hawa ni wazoefu na hawaendi kujifunza kuongoza. Mfumo wa kiuongozi katika nchi hii ni kwamba kiongozi wa juu ndiye mwenye maamuzi, ndiyo maana Wambura na Karia huwezi kuwahusisha na madudu yoyote yaliyopita TFF japo walikuwa madarakani.
    Maana yake Karia naye anapaswa kujifunza adha za uongozi wa ‘kimimi’ na kwenda kuongoza kwa pamoja na Kamati yake ya Utendaji katika mfumo mzuri wa uwajibikali wa pamoja.      
    Soka ya Tanzania ina makovu mengine, ambayo hapana shaka Wambura na Karia wanayajua na wanapaswa kwenda kuwa matabibu na si waongeza majeraha.
    Hatumkaribishi Karia TFF, kwa sababu alikuwepo na anaendelea kuwepo na Wambura naye anarejea baada ya miaka 12 na kwa pamoja wawili hao na Kamati yao nzima ya Utendaji tunawatakia kila la heri.
    Kufanikiwa kwao kiuongozi ndani ya shirikisho ni kufanikiwa kwa soka ya Tanzania – na watambue pia kufeli kwao kwa namna yoyote ni pigo lingine katika mchezo huo nchini. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA, WAMBURA SI WATU WAPYA KATIKA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top