• HABARI MPYA

    Saturday, August 12, 2017

    KARIA RAIS MPYA TFF, WAMBURA AWA MAKAMU

    Na Rehema Lucas, DODOMA
    WALLACE KARIA ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi uliofanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la St. Gasper mjini Dodoma.
    Karia amewashinda mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Ally Mayay, Katibu wa zamani wa shirikisho hilo, Frederick Mwakalebela, Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Wakili Imani Madega, Mwandishi wa Habari za Michezo wa zamani, Shija Richard na Katibu wa klabu ya Mbeya City, Emmanuel Kimbe.
    Michael Richard Wambura ameshinda nafasi ya Umakamu wa Rais akiwaangusha Mwenyekiti wa FA ya Dodoma, Mulamu Nghambi, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.

    Wallace Karia (kulia) akiwa na Michael Wambura baada ya matokeo kutangazwa leo ukumbi wa mikutano wa jengo la St. Gasper mjini Dodoma

    Karia amepata kura 95 kati ya 125 zilizopigwa, akifuatiwa na Mayay na Shija  waliopata kura 9 kila mmoja,  huku Wambura akipata kura 85 kati ya 125, akifuatiwa na Mulamu Nghambi aliyepata kura 25.
    Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Lameck Nyambaya kutoka Kanda ya Dar es Salaam aliyepata kura 41, akifuatiwa na Shaffi Dauda aliyepata kura 21, Khaled Mohammed kwa Kanda ya Kilimanjaro na Tanga aliyepata kura 70 na Fransis Ndulami kura 7O Kanda ya Pwani na Morogoro.
    Wengine ni Mohamed Ally 35 kanda ya Dodoma na Singida, Dunstan Ditopile kura 74 Kanda ya Lindi na Mtwara, James Mhagama kura 63 Njombe na Ruvuma, Elius Mwanjala kura 61 Mbeya na Ruvuma, Kenneth Pesambili 72 Katavi na Rukwa, Issa Bukuku kura 80 Kigoma na Tabora, Sara Chau kura 57 Manyara na Arusha, Mbasha Matutu kura 67 Shinyanga na Simiyu, Modestus  Lufanga kura 67 Mara na Mwanza, Salim Chama kura 92 Kagera na Geita.
    Baada ya matokeo hayo, washindi wote wa waliapishwa kwa agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe
    Ikumbukwe aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameshindwa kurudi kutetea nafasi yake baada ya kuweka rumande tangu Juni 29, mwaka huu kwa pamoja na Katibu weke, Selestine Mwesigwa na Isinde Isawafo Mwanga kwa tuhuma za ubadhirifu.
    Watatu hao walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
    Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani, lakini baada ya kesi hiyo kuanza kuunguurma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA RAIS MPYA TFF, WAMBURA AWA MAKAMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top