• HABARI MPYA

    Saturday, August 05, 2017

    AZAM FC YANG'ARA MCHEZO WA KIRAFIKI CHAMAZI, WAIKALISHA KMC 1-0

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAO pekee la beki Aggrey Morris limetosha kuipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Timu ya Manispaa ya Kinondoni, ijulikanayo kama KMC katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Ijumaa jioni.
    Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho wa kikosi hicho kabla ya kuelekea nchini Uganda kuweka kambi ya siku 10 katika maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya kuanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL),
    Nahodha huyo Msaidizi wa Azam FC, Aggrey Morris alifunga bao hilo dakika ya 57 kwa mkwaju wa penalti kufuatia mshambuliaji mpya, Wazir Junior kuangushwa kwenye eneo la hatari.
    Aggrey Morris akishangilia baada ya kufunga bao pekee dhidi ya KMC 
    Azam FC iliutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa hasa kipindi cha pili ikicheza soka safi la pasi na kasi huku ikishuhudiwa Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Junior, Enock Atta, Yahya Zayd, Bruce Kangwa, waking’ara vilivyo kwa kupeleka mashambulizi makali langoni mwa KMC.
    Ushindi huo ulikuwa zawadi nzuri kwa kocha Mromania, Aristica Cioaba aliyekuwa anasherehekea siku ya kuzaliwa Agosti 4 na baada ya mchezo huo akaenda kukata keki na wachezaji wake. 
    Huo ni mchezo wa tano kwa timu hiyo ya kocha Mromania, Aristica Cioaba katika mechi za kujiandaa na msimu mpya, ikiwa imeshinda mbili, sare moja na kufungwa mbili.

    Azam ilianza kwa kufungwa 4-2 na Rayon Sport mjini Kigali, Rwanda kabla ya kutoka sare ya 0-0  na Mbeya City mjini Mbeya, kufungwa 2-0 na Mji Njombe FC huko Makambako na kushinda 4-0 dhidi ya Lipuli mjini Iringa.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku moja kabla ya keshokutwa alfajiri kuanza safari ya kuelekea nchini Uganda itakapocheza mechi nne za kirafiki dhidi ya KCCA, Vipers, URA na SC Villa, zote zikiwa timu kongwe za nchini humo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YANG'ARA MCHEZO WA KIRAFIKI CHAMAZI, WAIKALISHA KMC 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top