• HABARI MPYA

    Tuesday, August 01, 2017

    AZAM FC WAENDA KUWEKA KAMBI UGANDA MAANDALIZI LIGI KUU

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    ZIKIWA zimesalia siku 25 kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kuanza, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuweka kambi ya siku 10 nchini Uganda kuanzia Jumapili ijayo Agosti 6 mwaka huu.
    Kambi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho Azam FC kuelekea msimu ujao wa ligi, ambapo mabingwa hao wamepangwa kuanza kutifuana na Ndanda ya Mtwara katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Agosti 26 mwaka huu.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo mjini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alisema kikosi hicho kikiwa nchini humo kinatarajia kucheza mechi nne kubwa za kirafiki na vigogo wa nchi hiyo, KCCA, SC Villa, Vipers na URA.
    “Kama manvyofahamu kuwa mazoezi yanakwenda na mechi za kirafiki za kujaribu na kuangalia kitu umefanya, kwa hiyo tutapokuwa Uganda tunatarajia kucheza na timu za KCCA, SC Villa, Vipers na URA, kadiri siku zitakavyokwenda tutazidi kuwapa tarehe za kucheza mechi hizo,” alisema.
    Alisema kikosi hicho kitakaporejea nchini Agosti 15 mwaka huu, kinatarajia kufanya maandalizi ya mwisho kabisa kabla ya ligi hiyo kuanza.
    Hiyo itakuwa ni ziara ya tatu ya Azam FC ya maandalizi, ya kwanza ilikuwa ni ile ya nchini Rwanda ilipokwenda kucheza na mabingwa wa Taifa hilo, Rayon Sports na kupoteza kwa mabao 4-2, na Alhamisi iliyopita ilimaliza ziara nyingine ya Nyanda za Juu Kusini.
    Katika ziara hiyo ya Nyanda za Juu Kusini, Azam FC ilicheza jumla ya mechi tatu za kirafiki, ikianza kutoka suluhu na Mbeya City, ikafungwa na Njombe Mji mabao 2-0 kabla ya kumaliza kwa kuichapa Lipuli ya Iringa mabao 4-0.
    Kipa mpya wa Azam FC, Razak Abalora, kutoka nchini Ghana aliyewasili Jumapili usiku naye anatarajiwa kuongozana na timu nchini humo.
    Abalora, 20, amesajiliwa na Azam FC akitokea WAFA SC ya Ghana, alikoiongoza timu hiyo kushika nafasi ya pili kwenye ligi hadi sasa huku akiwa na rekodi ya aina yake ya kucheza mechi 12 bila wavu wake kuguswa kati ya 22 alizocheza.
    Katika hatua nyingine, Azam FC imewatoa kwa mkopo wachezaji wake sita kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hao ni kipa Metacha Mnata anayekwenda Mbao pamoja na mshambuliaji Sadallah Mohamed, anayetokea kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC, huku mabeki wawili Godfrey Elias maarufu kama Albino na Abbas Kapombe wakienda Ndanda.
    Aidha, wachezaji wengine wawili waliokuwemo kwenye orodha hiyo ni Joshua John Thawe, aliyekwenda timu iliyopanda daraja ya Njombe Mji FC na Mudathir Yahya anayekwenda Singida United.
    Azam inaendelea na mazungumzo na baadhi ya timu ambazo zinamtaka kwa mkopo beki Ismail Gambo, moja ikiwa ya nje ya nchi na zingine za hapa nchini.
    Uamuzi wa kuwatoa nyota hao ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, lengo kubwa likiwa ni kuwapa fursa ya kucheza mechi nyingi zaidi ili kujijenga na hatimaye katika siku za usoni kurejea kikosini.
    Azam FC imekuwa na utamaduni wa kulinda vipaji vya wachezaji wake kupitia fursa hiyo, itakumbukwa kuwa kwa msimu miwili mfululizo tuliwatoa kwa mkopo wachezaji wetu kiungo Braison Raphael na winga Joseph Kimwaga.
    Wachezaji hao wamerejea hivi sasa wakiwa vizuri baada ya kukomaa vilivyo kupitia mechi walizokuwa wakicheza, hivyo tunaamini fursa hiyo itazidi kuwaendeleza wachezaji hao na kuwajenga zaidi huko waendapo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WAENDA KUWEKA KAMBI UGANDA MAANDALIZI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top