• HABARI MPYA

    Sunday, July 09, 2017

    KARIA AWAPONGEZA WASHINDI TWFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAIMU Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amewapa kongole viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake (TWFA), waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Chichi, Dar es Salaam.
    Katika uchaguzi huo uliopata uwakilishi wa theluthi mbili ya mikoa yote ya Tanzania, Amina Karuma alitetea kiti chake kwa kupata kura 47 kati ya 52 za wapigakura wote huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na Rose Kissiwa ambaye aliyepata kura 42.
    Mwanahabari Mkongwe wa Gazeti la Nipashe kutoka Jumba la Magazeti la The Guardian, Somoe Ng’itu alishinda nafasi ya Katibu Mkuu kwa kuvuna kura 49 ilihali Theresia Mung’ong’o alishinda nafasi ya Katibu Msaidizi. 
    Hilda Masanche alishinda nafasi ya Mweka Hazina wa TWFA kwa kupata kura 25 wakati Mwanahabari mwingine Zenna Chande alishinda nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kupata kura 44. 
    Wajumbe Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmine Soudy na Chichi Mwidege hawakushinda baada ya wagombea wote wanne kutopata zaidi ya nusu ya kura kulingana na idadi ya wapigakura kwa mujibu wa katiba ya TWFA. 
    Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Msomi Wakili George Mushumba, ambaye pia aliwapongeza washindi.
    Awali akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi aliwataka wajumbe hao kuwa makini katika kuchagua na kwamba si wakati wa kufanya mzaha katika soka la wanawake.
    Wakati huo huo: Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyokutana Julai 8, mwaka huu pamoja na mambo mengine pia ilijadili mchakato wa chaguzi za Mkoa wa Rukwa (RUREFA) na timu ya Lipuli inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom. 
    Kuhusu mchakato wa uchaguzi Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Kamati ya Uchaguzi inayoongozwa na Mwenyekiti Msomi Wakili Revocatus Kuuli, imeagiza zoezi hilo liendelee na inamtuma Mjumbe wake siku ya usaili, Msomi Wakili Thadeus Karua kwa ajili ya kushuhudia.
    “Na pia Kamati ya Uchaguzi itawatuma wajumbe siku ya uchaguzi tarehe 5 Agosti, 2017,” imesema kamati hiyo ilipoagiza kuhusu kuendelea kwa uchaguzi huo. 
    Kuhusu uchaguzi wa Lipuli,  Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Msomi Wakili Kuuli, imemwagiza Katibu Mkuu wa klabu hiyo, kuendelea na maandalizi ya uchaguzi kama ilivyoelekezwa na kamati kwamba ufanyike Agosti 5, mwaka huu.
    “Na Kamati inamtuma mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi Msomi Wakili Mohamed Ally Mchungahela kwa ajili ya uangalizi siku ya uchaguzi,” imesema sehemu ya taarifa ya kamati kwa uongozi wa Lipuli.
    Kamati imesisitiza, “Na wanachama waendelee kulipia ada za uanachama kwa kuwa watakaoruhusiwa kupiga kura ni wanachama hai tu.”
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA AWAPONGEZA WASHINDI TWFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top