• HABARI MPYA

  Wednesday, June 14, 2017

  SIMBA YASAJILI KIPA WA MBAO MIAKA MIWILI, AISHI…

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  WAKATI mashabiki wa timu wakisubiri kwa hamu klabu yao imtambulishe kipa namba moja Tanzania kwa sasa, Aishi Salum Manula, leo Simba SC imemtambulisha mlinda mlango wa tatu wa Mbao FC ya Mwanza, Emmanuel Elias Mseja kama mchezaji wa tano rasmi kusajiliwa.
  Habari zimevuja, Simba imemsajili Tanzania One, Aishi Manula kutoka Azam FC, lakini bado klabu hiyo haijamtambulisha rasmi kama ilivyofanya kwa wachezaji wengine, mabeki Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC pia, Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans ya Mwanza iliyoshuka Daraja, Shomary Kapombe na mshambuliaji John Bocco kutoka Azam FC. 
  Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' (kushoto) akimkabidhi jezi ya klabu hiyo, kipa Emmanuel Elias Mseja kutoka Mbao baada ya kusiani mkataba wa miaka miwili

  Mseja aliyesaini mkataba wa miaka miwili Simba SC, alikuwa kipa wa akiba wakati wote msimu uliopita Mbao FC, baada ya Erick Ngwengwe na Benedict Haule waliodaka kwa awamu.
  Ngwengwe alikuwa kipa wa kwanza wa Mbao FC kabla ya kufukuzwa kufuatia kufungwa mabao matatu rahisi ndani ya dakika 10 za mwisho za mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba, iliyotoka nyumba kwa 2-0 na kushinda 3-2 Aprili 10, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
  Baada ya hapo, Benedict akadaka mechi zilizosalia na kumalizia vizuri msimu, akiiwezesha timu kwanza kubaki Ligi Kuu na pia kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 27, ikifungwa na Simba 2-1 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
  Na Mseja anakwenda kuwa kipa wa nne Simba, mbali ya Aishi Manula, wengine Mghana Daniel Agyei aliye hatarini kuachwa na wazalendo, Peter Manyika na Dennis Richard wote mazao ya Simba B.   
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YASAJILI KIPA WA MBAO MIAKA MIWILI, AISHI… Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top