• HABARI MPYA

    Friday, June 16, 2017

    RAIS MALINZI AMPA 'MKONO WA KWAHERI' MGOYI

    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, Ahmed 'Msafiri' Mgoyi kwa utumushi mara baada ya kutangaza kutowania nafasi yoyote ya uongozi.
    Mjumbe Mgoyi anayewakilisha Mikoa ya Kigoma na Tabora aliandika waraka jana Juni 15, 2017 akielezea kutogombea tena katika Uchaguzi wa TFF unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
    “Nimefanya kazi na Wajumbe wangu wote wa Kamati ya Utendaji. Tumefanya kazi kwa uadilifu mkubwa. Wakati Tukielekea kwenye uchaguzi, mwenzetu ametangaza kutogombea tena, lakini kwa namna nilivyofanya naye kazi, kwangu mimi naamini anahitajika mno, lakini uamuzi wake ni mwisho unakuwa ni wa kwao.

    Rais wa TFF, Jamal Malinzi wa pili kushoto akiwa na rais wa zamani wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga mjini Sao Paulo, Brazil kushiriki Mkutano Mkuu wa 64 wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwaka 2014. Wengine kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyi  na kushoto ni katibu wa shirikisho hilo, Celestine Mwesigwa

    “Naamini kwamba bado ni mwanafamilia wa mpira wa miguu na pindi atakapohitajika kwa lolote lile kama vile ushauri na masuala mengine, basi hatutasita kuwafuata kwa sababu lengo ni kujenga na kuendeleza mpira wetu,” amesema Malinzi.

    Katika ujumbe wake, Rais Malinzi amesema kwamba hadhani kama Mgoyi hao atasita au kukataa kutoa ushirikiano kwa uongozi wa shirikisho pindi akihitajika kutoa msaada wao wa mawazo na ushauri.
    Rais Malinzi amemtakia kila la kheri katika majukumu yake mengine aliyojipangia kuyafanya huku akiwa bado mwanafamilia wa mpira wa miguu.
    Katika hatua nyingine, TFF imerahisishia namna ya kupata fomu za kugombea uongozi katika uchaguzi wake Agosti 12, mwaka huu baada ya tovuti ya TFF (www.tff.or.tz) kuwa kwenye marekebisho.
    "Kwa wanafamilia ambao wapo nje ya Dar es Salaam, wanaotaka fomu hizo kwa sasa hawana budi kutuma ujumbe wa barua pepe kwenda kwenye anwani ya info@tff.or.tz na moja kwa moja atajibiwa kwa kupata fomu hizo ziliazoanza kutolewa leo Juni 16, mwaka huu. Kwa walioko Dar es Salaam, wanaweza kupata fomu hizo katika ofisi za TFF zilizo Karume, Ilala jijini Dar es Salaam,".
    "Mwanafamilia wa mpira wa miguu mwenye nia ya kugombea ataweza kufungua fomu hizo na kuzijaza huku akifuata utaratibu wa kulipia kwenye nambari ya akaunti 01J1019956700 katika Benki ya CRDB,".
    Zoezi hili kuchukua fomu na kuzirejesha fomu lililoanza leo Juni 16, litafikia kikomo Juni 20, mwaka huu kwa mujibu wa Kanuni ya 10.8 ya Uchaguzi kama ilivyoanishwa kwenye katiba ya TFF.
    Mara baada ya kulipia, Mgombea atawajibika kuwasilisha stakabadhi ya malipo kutoka benki na kupewa fomu ya nafasi husika.
    Gharama za kuchukulia fomu ni. Sh 500,000 kwa Urais, Sh. 300,000 Makamu wa Rais na Sh. 200,000 kwa Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
    Wakati huo huo: Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi, amempongeza Francis Amin Michael kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan Kusini (SSFA).
    Amin - Mfanyabiashara aliyepata kuwa Mjumbe wa Bodi ya timu Atlabara FC, alishinda nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Juba ambako aliwashinda Lual Maluk Lual na Arop Joh Aguer baada ya kuvuna kura 22 kati ya 34.
    Amin anamrithi Chabur Goc Alei, ambaye hakutetea nafasi hiyo.
    Katika salamu za pongezi, Rais Jamal Malinzi amesema kwamba ana imani na Amin katika nafasi hiyo kwa kuwatumikia vema Wana Sudan Kusini kama alivyoahidi mara baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
    Rais Malinzi anaamini kwamba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Serikali ya Sudan Kusini, ataendeleza mpira wa miguu hususani katika Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ambako Tanzania na Sudan Kusini ni nchi wanachama. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MALINZI AMPA 'MKONO WA KWAHERI' MGOYI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top