• HABARI MPYA

    Thursday, June 01, 2017

    MWAKYEMBE: UJIO WA EVERTON NI FURSA NZURI KWA KLABU ZETU

    Na Zainab Ramadhani, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema kwamba ujio wa klabu ya Everton nchini ni fursa nzuri kwa klabu za Tanzania kujifunza. 
    Akizungumza leo asubuhi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika hafla maalum ya kutambulisha rasmi ziara hiyo ya kihistoria, Waziri Mwakyembe amesema kwamba Everton ni timu kubwa na kongwe katika soka ya Uingereza ikiwa na miaka zaidi ya 140 tangu kuanzishwa kwake.
    Amesema kwamba ujio wake nchini ni mwanzo mzuri kwa klabu za Tanzania kupata muda wa kuona na kujifunza kwa wenzetu namna ya kuendesha klabu kisasa.
    Waziri wa Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (kulia) akimshuhudia mchezaji wa zamani wa Everton, Leon Osman akisalimiana na wachezaji vijana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo 

    Mwakyembe amesema, mbali na klabu kujifunza na hata wachezaji pia wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujitangaza na kuacha kuridhika na umaarufu wanaoupata kutoka katika timu za Simba na Yanga.           
    Mapema leo kampuni ya SportPesa imethibitisha ujio wa wapinzani hao wa Everton nchini Tazania mwezi ujao katika ziara ya mchezo maalum mmoja wa kirafiki.
    Mkurugenzi Mtendaji wa Everton, Robert Elston alikuwepo kwenye utambulisho wa ziara hiyo na akasema kwamba wanakuja nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza mechi hiyo ya kirafiki itakayofanyika Julai 13 ikiwa ni siku mbili baada ya kumalizika michuano ya SportPesa Super Cup.
    Elston ameongozana na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Leon Osman ambaye alishiriki uzinduzi wa programu ya timu za vijana nchini, itakayosimamiwa na SportPesa.
    Michuano ya SportPesa Super Cup inatarajiwa kushirikisha timu nane, nne kutoka Kenya ambazo ni AFC Leopards, Gor Mahia, Tusekr na Nakuru All Stars, Simba, Yanga, Singida na  Jangombe boys.
    Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Juni 5, mwaka huu hadi Juni 11 na itafanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam na bingwa ndiye atakayemenyana na Everton inayoongozwa na mkali wa mabao wa Ubelgiji, Romelu Lukaku.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAKYEMBE: UJIO WA EVERTON NI FURSA NZURI KWA KLABU ZETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top