• HABARI MPYA

    Friday, June 02, 2017

    MALINZI: TUTAANDAA FAINALI NZURI NA ZA KIHISTORIA ZA U-17 AFRIKA

    Na Mwandisi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema kwamba Tanzania itaandaa fainali nzuri na za kihistoria za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka mwaka 2019.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam leo, Malinzi amesema kwamba baada ya Tanzania kupewa uenyeji wa AFCON ya U-17 mwaka 2019 nguvu zinapelekwa kwenye maandalizi. 
    “Tarehe 28 Mei 2017, baada ya mchezo wa fainali za AFCON U-17, Rais wa CAF (Shirikisho la Soka Afrika), Ahmad aliikabidhi rasmi Tanzania uenyeji huu kwa njia ya ishara ya kumkabidhi Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa bendera ya CA, tukio ambalo lilishuhudiwa na dunia nzima,”amesema Malinzi.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo
    Rais huyo wa TFF amesema kwamba taratibu za kuandaa fainali hizo zitaratibiwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya TFF na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo. “Ni Imani ya Shirikisho kuwa Tanzania itaandaa fainali nzuri na za kihistoria. TFF inatoa rai kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania tushirikiane ili tuzitumie fainali hizi kujenga jina la nchi yetu kimichezo, kiutamaduni, kiutalii na kiuchumi,” amesema.
    Kwa kuwa mwenyeji, Tanzania itacheza moja kwa moja fainali hizo za Afrika, hiyo ikiwa mara ya pili mfululizo na Malinzi amesema jitihada zitafanyika kuhakikisha kombe hili linabakia nyumbani.
    Amesema maandalizi ya timu itakayoshiriki fainali hizo yalianza mwaka 2015 kwa TFF kuendesha mashindano ya kitaifa ya vijana umri chini ya miaka 13 (U13) na katika awamu ya kwanza ya maandalizi hayo, vijana 22 bora waliopatikana kwenye mashindano haya walikusanywa pamoja na kwa ruhusa ya wazazi wao walipatiwa shule ya kusoma pamoja ambapo wanapata fursa ya kusoma na kufanya mazoezi ya pamoja. 
    “Shule hii iko mjini Mwanza. Awamu ya pili itakayoanza mwezi Julai itahusisha vijana hawa kuongeza kasi ya mazoezi na hivyo itabidi wasome katika shule iliyokaribu na benchi la ufundi la timu hii ambayo sasa ndiyo rasmi Serengeti Boys. Shule hii tayari imekwisha patikana hapa Dar es Salaam na taratibu za masomo yao zinaandaliwa,”amesema Malinzi. 
    “Tunawashukuru wazazi wa watoto hawa kwa kutoa ushirikiano kwetu, pia tunaishukuru shule ambayo wamekuwa wakisomea kwa ushirikiano wao. Mwezi Julai timu hii itacheza mechi mbili za majaribio za kimataifa. Imani ya TFF ni kuwa tutajenga kikosi imara cha Serengeti Boys mpya ambacho kitatoa ushindani na kunyakua kombe la Afcon U17 mwaka 2019,” ameongeza.
    Awali ya hapo, Malinzi alitoa shukrani za kwa wadau mbalimbali kuichangia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za mwaka huu za Afrika nchini Gabon mwezi uliopita.  
    “Timu yetu ya Taifa ya vijana umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys ilishiriki katika fainali hizi na kutolewa hatua ya makundi. Katika hatua hii ilitoa sare ya 0-0 dhidi ya Mali, ikaifunga Angola bao 2-1 na kutolewa kwa sheria ya uwiano wa matokeo (head to head) baada ya kufungwa bao moja kwa bila na Niger,”.
    “Ni jambo la kutia moyo kuwa bingwa wa mashindano haya Mali timu pekee ambayo hawakuweza kuifunga ni Tanzania na timu nyingine zote walizokutana nazo walizifunga ikiwemo na Ghana ambayo Serengeti Boys walitokana nayo sare hapa Dar es salaam,” amesema.
    Malinzi amesema mashindano ya Gabon yameonyesha Tanzania ina uwezo mkubwa wa kushindana katika mashindano makubwa na wao kama TFF wanamshukuru mno Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri  Mkuu Mh Kassim Majaliwa ambao kwa umoja wao walihakikisha timu inawezeshwa kikamilifu na kuwa na nguvu kubwa ya kushindana.
    Wamemshukuru pia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe pamoja na watumishi wa Wizara kwa ushirikiano na jitihada kubwa walizozifanya kuhakikisha timu inapata maandalizi mazuri.
    “Tunawapa hongera na kuwashukuru wachezaji wa Serengeti Boys kwa jitihada na ukomavu wao katika kipindi cha maandalizi na cha fainali zenyewe. Pongezi nyingi na shukrani kwa benchi la ufundi la timu na uongozi wa timu unaoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayoub Nyenzi, Kamati ya Utendaji ya TFF wakati wote ilikuwa karibu naye na ilimpa nguvu sana,”amesema Malinzi. 
    Amesema Serengeti Boys iliyochoshiriki fainali za Gabon inabadilika na kuwa rasmi timu ya vijana umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes ambayo mwakani itashiriki katika hatua hatua za kufuzu kucheza fainali za Afrika umri chini ya miaka 20 Afcon U20, zitakazofanyika mwaka 2019. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI: TUTAANDAA FAINALI NZURI NA ZA KIHISTORIA ZA U-17 AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top