• HABARI MPYA

    Saturday, June 03, 2017

    KARIBU TENA BECKHAM, HII NDIYO TANZANIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KWA mara nyingine, Tanzania ilipata ugeni mzito kupitia sekta ya utalii, kufuatia ujio wa Nahodha wa zamani wa England, David Robert Joseph Beckham aliyewasili nchini Mei 27, mwaka huu kabla ya kuondoka leo, Juni 3.
    Beckham alikuwa nchini kwa wiki moja na kuzuru katika vivutio mbalimbali vya kiutalii ikiwemo mbuga ya wanyama ya Serengeti pamoja na familia yake, mkewe, Victoria Adams ‘Posh’ na wanawe, Brooklyn Joseph, Romeo James, Cruz David na Harper Seven.
    Bahati mbaya, ziara yake, kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, Preston North End, Real Madrid, AC Milan, LA Galaxy na Paris Saint-Germain hakutaka iingiliwe na vyombo vya Habari.
    David Beckham (kulia) akiwa na mwanawe mkubwa, Brooklyn katika mbuga ya Serengeti

    Beckham akibusu na binti yake mdogo, Harper Seven walipokuwa Serengeti 
    Harpe Seven akitazama wanyama kupitia kifaa maluum
    David Beckham akiwa ametulia na glasi yake ya mvinyo kwenye mbuga ya Serengeti
    Beckham akiwa na mwanawe mkubwa, Brooklyn Joseph
    Mtoto mwingine wa kiume wa Becks, Cruz akiwa ametulia katika kijua cha asubuhi mbuga ya Serengeti

    Aliifanya siri kubwa kuanzia wakati anatoka Uingereza hadi kuwasili kwake, Dar es Salaam na bahati nzuri kwake, wenyeji wake, yaani kampuni ya utalii iliyompokea na kumtembeza nchini ilikuwa ina uadilifu wa hali ya juu kwa kutovujisha kwenye vyombo vya habari ujio wake.
    Na hatimaye Becks, kama alivyokuwa akipenda kuitwa enzi za ujana wake akicheza soka ya ushindani amekuwa na wiki moja nzuri na tulivu katika viunga vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuondoka leo.
    Watu wa kwanza kuvujisha habari za uwepo wa Becks nchini ni wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam walioanza kusambaza picha yake wakati anawasili uwanjani hapo.
    Walipata picha moja tu na kurekodi kipande kidogo mno cha video, akiteremka kwenye ngazi za mlango wa kutokea watu maalum (VIP) eneo la JNIA.
    Na tangu hapo, haikuonekana tena picha ya Becks zaidi ya zile alizopost mwenyewe kwenye ukurasa wake wa Instagram. 
    Ulikuwa mgeni mzito, kwa sababu Beckham ni mmoja wa wanasoka wakubwa kuwahi kutokea duniani, akiwa anajivunia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa England kushinda mataji ya Ligi Kuu za nchi nne; England, Hispania, Marekani na Ufaransa kabla ya kustaafu soka Mei 2013 baada ya miaka 20 ya kuwa uwanjani na kushinda mataji 19.
    Akiwa anafahamika kwa utoaji wake wa pasi nzuri na kupiga vizuri mipira iliyokufa enzi zake akicheza wingi ya kulia, Beckham alishika nafasi ya pili mara mbili katika tuzo ya Mwanasoka Bpra wa Dunia, maarufu kama Ballon d'Or.
    Kisoka, Beckham aliibukia Manchester United, ambako alianza kuchezea kikosi cha kwanza mwaka 1992 akiwa ana umri wa miaka 17 na akafanikiwa kushinda mataji sita ya Ligi Kuu yaa timu hiyo na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.
    Baada ya hapo akaenda kucheza kwa misimu minne Real Madrid, akishinda taji la La Liga katika msimu wake wa mwisho na klabu hiyo.
    Julai mwaka 2007 akasaini mkataba wa miaka mitano na LA Galaxy ya Marekani na akiwa huko, akaenda kucheza kwa mkopo Italia mara mbili mwaka 2009 na 2010. Na piaanajivunia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Muingereza kucheza mechi 100 za Ligi ya Mabingwa.
    Kwenye soka ya kimataifa, Beckham aliichezea kwa mara ya kwanza England Septemba 1, mwaka 1996 akiwa ana umri wa miaka 21 kabla ya kuwa Nahodha kwa miaka sita akicheza jumla ya mechi 58 zikiwemo za Kombe la Dunia 1998, 2002 na 2006, na fainali mbili za Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2000 na 2004.
    Huyo ndiye Becks na alikuwa Tanzania kwa wiki moja. Karibu tena Beckham, hii ndiyo Tanzania, wasalimie wote, waambie na wao wanakaribishwa pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIBU TENA BECKHAM, HII NDIYO TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top