• HABARI MPYA

    Saturday, April 08, 2017

    YANGA YAPIGA HODI MAKUNDI AFRIKA, YAWACHAPA WAARABU 1-0

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    BAO pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko limeipa Yanga ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Rasta huyo alifunga bao hilo dakika ya 61 akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa baada ya kazi nzuri ya kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima aliyepasua na  mpira kutokea nyuma.
    Yanga sasa itahitaji sare katika mchezo wa marudiano wiki ijayo mjini Algiers. Algeria ili kwenda hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho kwa mara ya pili mfululizo mwaka huu.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa kutoka Rwanda, Louis Hakizimana aliyeyepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka, Yanga ilipoteza nafasi nzuri zaidi ya tatu za kufunga kipindi cha kwanza.
    Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Thabani Kamusoko (wa pili kulia) baada ya kufunga bao pekee dakika ya 61  
    Kiungo wa Yanga, Obrey Chirwa akimtoka beki wa MC Alger, Kacem Mehdi
    Beki wa Yanga, Hassan Kessy akimtoka beki wa MC Alger, Kacem Mehdi
    Winga wa Yanga akimtoka beki wa MC Alger, Kacem Mehdi
    Thabani Kamusoko akiwa chini baada ya kuangushwa na wachezaji wa MC Alger  
    Beki wa Yanga, Mwinyi Hajji Mngwali akipambana na mchezaji wa MC Alger

    Baada ya mchezo kuanza taratibu kwa timu zote kusomana, MC Alger walikuwa wa kwanza kulijaribu lango la Yanga baada ya shuti la Goveri Kaled kudakwa na kipa Chaouch Faruzi.
    Yanga waliotumia mfumo wa 4-3-3 wakishambulia na Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wakalitia majaribu kwa mara ya kwanza lango la MC Alger dakika ya 15, lakini kiungo Haruna Niyonzima akachelewa kuiwahi krosi ya beki Hassan Kessy. 
    Baadaye Yanga wakabadilika na Kaseke akarudi kucheza kama kiungo huku Kamusoko akisogea katikati kucheza kama mshambuliaji pacha wa Chirwa na hapo ndipo mabingwa hao wa Tanzania walipoanza kuwaamsha mashabiki wao kwa kosa kosa za kusisimua.
    Winga Simon Msuva alitia krosi nzuri dakika ya 29, lakini mshambuliaji Obrey Chirwa akapiga fyongo mpira ukapotelea kwenye himaya ya wapinzani na kuondoshwa kwenye hatari. 
    Msuva tena akatia krosi dakika ya 28 na pamoja na kumfikia kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko akapiga nje akiwa kwenye boksi. 
    Chirwa naye akapata pasi nzuri ya Mwinyi Hajji Mngwali upande wa kushoto wa Uwanja dakika ya 44, akaingia ndani vizuri na kupiga shuti zuri, lakini likaende nje upande wa pili wa lango sentimina chache tu.                          
    Kamusoko tena akaikosesha Yanga bao dakika ya 45 na ushei baada ya kupiga juu ya lango kufuatia pasi nzuri ya Msuva.
    Kipindi cha pili, kocha Mzambia wa Yanga alianza na mabadiliko akimpumzisha kiungo Deus Kaseke na kumuingiza mshambuliaji Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma aliyekwenda kuongeza kasi ya mashambulizi ya wan Jangwani.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munish ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Haruna Niyonzima/Emanuel Martin dk82 na Deus Kaseke/Donald Ngoma dk56.
    Mo Alger; Chaouch Faruzi, Hachoud Abdullman, Karaovi Amir, Mebarakou Zidane, Bouhenna Richid, Kacem Mehdi, Chrifei Hichem, Bougueche Hajj/Feedbad Zahir dk85, Derarya Warid/Awady Said dk76, Goveri Kaled/BemmouAbdulcheri dk74 na Nekkache Hichem. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAPIGA HODI MAKUNDI AFRIKA, YAWACHAPA WAARABU 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top