• HABARI MPYA

  Friday, April 14, 2017

  VITA YA UBINGWA LIGI KUU YAHAMIA MEZANI, YANGA NAO WATAKA POINTI ZA AFRICAN LYON

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  VITA ya ubingwa wa taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara sasa imehamia mezani, baada ya mabingwa watetezi Yanga SC nao kuibua malalamiko ya pointi za chee dhidi ya African Lyon.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam leo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi amesema kwamba wanawakumbusha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji madai yao dhidi ya African Lyon kumchezesha Venance Ludovick wa Mbao FC.
  “Napenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwamba na sisi tuna malalamiko yetu Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji dhidi ya African Lyon kumchezesha Venance Ludovick wa Mbao FC katika mechi baina yetu na wao,”amesema Mkemi.
  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam leo

  Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
  Katika mchezo huo ambao Kagera Sugar walishinda mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, wanadaiwa kukiuka kanuni kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano. 
  Ushindi wa rufaa hiyo unaifanya Simba ifikishe pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, wakiendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 za mechi 25.
  Ijumaa ya Desemba 23, mwaka jana mchezaji Ludovic aliichezea African Lyon katika mechi dhidi ya Yanga Uwanja wa Uhuru timu hizo zikitoka sare ya 1-1 wakati akiwa mchezaji halali wa Mbao FC.
  Hata hivyo, Kamati ya Saa 72 ikashindwa kuyatolea uamuzi malalamiko ya Yanga kwa madai mchezaji huyo alipewa leseni kimakosa na Ofisa wa TFF, ambaye hakutajwa jina.
  Lakini baada ya hapo, mchezaji huyo alizuiwa kucheza Ligi Kuu, hali inayoashiria hata Yanga wanaweza kuvuna pointi za mezani iwapo watatilia mkazo malalamiko yao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VITA YA UBINGWA LIGI KUU YAHAMIA MEZANI, YANGA NAO WATAKA POINTI ZA AFRICAN LYON Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top