• HABARI MPYA

    Friday, April 14, 2017

    KAGERA SUGAR WAINUKA, WATINGA TFF KUTAKA WAREJESHEWE POINTI ZAO WALIZOPEWA SIMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Kagera Sugar ya Bukoba imetuma barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia timu hiyo kwa madai ya kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
    Katika barua iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki kuelekea kwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, klabu hiyo imeliomba shirikisho hilo kupitia upya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyodaiwa.
    “Ndugu Katibu Mkuu klabu ya Kagera Sugar inapinga vikali maamuzi haya, kwani tunapenda kukuthibitishia kuwa kutokana na kumbukumbu zetu, mchezaji huyo Mohammed Fakhi hakuwa na kadi tatu kabla ya mchezo huo wa tarehe 2/4/2017 bali alikuwa ana kadi mbili alizoonyeshwa kwenye michezo yetu dhidi ya Mbeya City na Maji Maji ambayo ilichezwa huko nyuma,”amesema Madaki.
    Kagera inapinga uamuzi huo wa Kamati ya Saa 72 siku moja tu baada ya kutolewa jana usiku, kufuatia kikao chake kilichofanyika makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo ambao Kagera Sugar walishinda mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wanadaiwa kukiuka kanuni kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano. 
    Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Mohammed Yahya aliwaambia Waandishi wa Habari jana usiku Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kwamba Kamati ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake ni kupokonywa ushindi.
    Kwa ushindi huo wa mezani, Simba sasa imefikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, wakiendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 za mechi 25.
    Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Katika kikao chake awali Ijumaa iliyopita, Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, iliahirisha shauri hilo hadi leo kujipa muda wa kufuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo..
    Tayari taarifa zinasema Viongozi wa Kamati ya Saa 72 wameitwa Kamati ya Nidhamu kujieleza juu ya maamuzi hayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAGERA SUGAR WAINUKA, WATINGA TFF KUTAKA WAREJESHEWE POINTI ZAO WALIZOPEWA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top