• HABARI MPYA

  Wednesday, April 19, 2017

  SIMBA WAITUPIA ZIGO LA LAWAMA TFF, WADAI KUNA HUJUMA WANAFANYIWA

  Na Steven Kinabo, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba imedai kwamba inafanyiwa njama na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili isitimize dhamira yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, Msimbazi, Dar ea Salaam kwamba wamegundua kuna njama za waziwazi zinafanywa na baadhi ya vigogo wa TFF ili kuwabeba Yanga.
  “Sisi kama Simba, tumegundua mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya watu pale TFF, wanachotaka wao ni klabu yetu ikose ubingwa ili Yanga wauchukue na kwa taarifa yenu ni kwamba tunajua kila kitu kinachoendelea na hatutakubali kukaa kimya.
  “Tunazo taarifa kwenye kile kikao cha kwanza cha Saa 72, mmoja wa viongozi wakuu wa TFF alitoa taarifa kwa mmoja wa maofisa wake akishinikiza matokeo yale yasitangazwe, ushahidi tunao, tunasubiri mamlaka halali tuuweke hadharani, ila bodi ikakataa na ikasema hiki ni kikao halali huyo ofisa yupo, tunalitaka jeshi na mamlaka nyingine kama TCRA vichunguze sakata hili,”alisema.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar ea Salaam 

  Alisema kama wakipokonywa pointi za mezani walizopewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kutokana na Rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu watalipeleka suala hilo ngazi za juu.
  Manara amesema anaona hawatendewi haki kwa sababu Rais wa TFF, Jamal Malinzi ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), hivyo anataka kuibeba timu ya mkoa wake.
  Kuhusu malalamiko ya Kagera Sugar dhidi ya maamuzi ya Saa 72, Manara amesema; “Haya malalamiko hayana uhalali wa kusikilizwa, ilikuwa yarudishwe kwenye bodi ya Ligi ili ifanye marejeo na wala haikuhitaji ushahidi mpya, utaratibu wa marejeo ni kutumia ushahidi ule ule wa mara ya kwanza,”alisema.
  Manara alikwenda mbali kwa kuishangaa kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji kuwahoji watu ambao hawahusiki kwa kwenye maamuzi hayo.
  “Eti mchezaji anaitwa kuhojiwa, yaani mwizi anaulizwa eti una kadi, Mgosi alipokuwa anacheza Simba ikanyang’anywa pointi hakuitwa popote, Erasto Nyoni naye hivyo hivyo, haijawahi kutokea popote duniani alafu unamuita mwamuzi wa akiba ambaye ametoka mkoa wa Kagera, hana ripoti atakwambia nini? Unadhani hii ni kuionea Simba,”alisema.
  Alisema kuwa sakata hilo kwa sasa limepelekwa kwenye makosa ya mtandaoni (Cybercrime) ambalo ipo chini ya jeshi la polisi kwa madai kuwa email iliyotumwa na mwamuzi imefojiwa.
  “Hivi ripoti zote za waamuzi zimeshawahi kwenda Cybercrime? Kuna kesi pale? Ni kutuonea kulikovuka mpaka kwa nini isiende na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)? kwanini lisiende kwenye vyombo vingine vinavyosimamia kama IT, kama wanataka usawa basi viitwe vyombe vya nje yaani wanatakiwa kutuomba radhi yaani kutuhusisha tu, kwamba tunaweza kufoji wametukosea,”alisema.
  Alisema kuwa msimamo wa Simba kwenye sakata hilo ni kamati hiyo kuwaomba radhi kwa kuwadhalilisha 
  “Tuombwe radhi, kutuhusisha tu au kututuhumu wametukosea sana sisi tuna uhakika wa asilimia zaidi ya 100 hivi email unachezeaje? Boniface Wambura mnayemjua uwezo alionao atakubali kuchezea address yake? Huku ni kutuonea kwa manufaa ya kuibeba Yanga tu,”alisema.
  Manara alikwenda mbali zaidi kwa kukumbushia kesi ya mshambuliaji wao Ramadhani Singano ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Azam.
  “Yaani kesi yetu toka Julai 2015 mpaka leo kimya, kamati hiyo hiyo iliyopeleka Cybercrime imeshindwa tukataka na review hawajajibu,”amesema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WAITUPIA ZIGO LA LAWAMA TFF, WADAI KUNA HUJUMA WANAFANYIWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top