• HABARI MPYA

  Saturday, April 15, 2017

  SIMBA INA KAZI NA TOTO LEO KIRUMBA

  Na Steven Kinabo, MWANZA
  VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC wanateremka Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kumenyana na Toto Africans katika mfululizo wa ligi hiyo.
  Simba wapo Mwanza kwa zaidi ya wiki nzima na Jumatatu wiki hii walicheza na wana mkoa huo wengine, Mbao FC na kushinda 3-2.
  Simba inataka kuweka rekodi ya kuchukua pointi zote sita mjini Mwanza kwa kuifunga na Toto pia leo, ili kusafisha njia yake kuelekea kwenye taji la ubingwa wa Ligi Kuu.
  Lakini halitarajiwi kuwa jepesi mbele ya Toto, ambayo iko hatarini kuipa mkono wa kwaheri LIgi Kuu na inapambana kuepuka kushuka.
  Na zaidi ni kwamba Toto yenye maskani yake Mtaa wa Kishamapanda, Mwanza inataka kulipa kisasi cha kufungwa 3-0 na Simba kwenye mchezo wa kwanza Oktoba 23, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 61 baada ya kucheza mechi 26, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 za mechi 25.
  Na hiyo imefuatia juzi kupewa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
  Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 iliipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu baada ya kujiridhisha Kagera Sugar ilimtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano.
  Hata hivyo, jana Kagera Sugar imetuma barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga uamuzi huo wakidai mchezaji wao alikuwa sahihi kucheza na hivyo wanataka kurejeshewa ushindi wao.
  Katika barua iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki kuelekea kwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, klabu hiyo imeliomba shirikisho hilo kupitia upya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyodaiwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA INA KAZI NA TOTO LEO KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top