• HABARI MPYA

    Saturday, April 15, 2017

    KILA LA HERI YANGA DC ALGERIA, MECHI INAANZA SAA 2:00 USIKU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC wanateremka kwenye Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Al-Jaza’ir, Algiers kumenyana na wenyeji, Mouloudia Club Alger katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania tiketi ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Mchezo huo unatarajiwa kuanza Saa 2:00 usiku unatarajiwa kuwa mkali kutokana na kile kilichoonekana kwenyee mchezo wa kwanza kwamba timu hizo hazipishani sana kwa viwango.
    Yanga ilishinda 1-0 mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na leo itahitaji sare tu ili kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili mfululizo. 
    Mwaka jana pia, Yanga pia ilicheza hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola ikitoka kutolewa na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa. 
    Katika mchezo wa leo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa aliyecheza vizuri mechi ya kwanza Dar es Salaam. Mzambia huyo peke yake amegomaa kushinikiza alipwe mishahara ya miezi mitatu. 
    Lakini habari njema ni kwamba, washambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu wote wamesafiri na timu. 
    Yanga iliondoka kwa awamu mbili Alhamisi mjini Dar es Salaam, kundi la kwanza likiondoka Saa 10;00 jioni kwa ndege ya shirika la Emirates kupitia Dubai na kundi la pili Saa 2:00 usiku kwa ndege ya shirika la Uturuki kupitia Istanbul.
    Kundi la kwanza lilikuwa na mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Hassan Kessy, viungo Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe.
    Katika kundi hilo, kulikuwa benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, Msaidizi wake, Juma Mwambusi, Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Noel Mwandila pia wa Zambia, kocha wa makipa, Juma Pondamali, pamoja na Meneja Hafidh Ally, Daktari Edward Bavu na Mchua Misuli, Jacob Onyango.   
    Kundi la pili lilikuwa na makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Beno Kakolanya; mabeki; Juma Abdul, Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Vincent Bossou na Kevin Yondan.
    Viungo ni Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Emmanuel Martin wakati mshambuliaji ni Donald ngoma.  
    Kocha Mkuu, George Lwandamina ana matumaini sana ya kumalizia vizuri mchezo wa leo na kusonga mbele, akijivunia rekodi ya kutopoteza mechi hata moja hadi sasa kwenye michuanio ya Afrika akitoa sare tatu na kushinda mmoja.
    Kila la heri Yanga SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI YANGA DC ALGERIA, MECHI INAANZA SAA 2:00 USIKU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top