• HABARI MPYA

  Wednesday, September 21, 2016

  ULIMWENGU: NATAKA KUBEBA KOMBE LA SHIRIKISHO PIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba atafurahi kuinua na Kombe la Shirikisho Afrika pia akiwa na klabu yake, TP Mazembe ya DRC baada ya mwaka jana kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa. 
  “Nimeyapokea kwa furaha matokeo ya sare ya ugenini katika Nusu Fainali ya Kwanza, na ninaamini sasa tutashinda nyumbani na kwenda fainali,”alisema Ulimwengu, ambaye alishindwa kusafiri na Mazembe kwenda Tunisia kutokana na pasipoti yake kwisha.
  Thomas Ulimwengu akiichezea Taifa Stars dhidi ya Misri
  Mazembe ilibisha hodi Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kulazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya wenyeji, Etoile du Sahel Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia usiku wa Jumamosi.
  Na Ulimwengu hakusafiri na mabingwa hao wa mwaka jana Afrika kutokana na kulazimika kurejea nyumbani kushughulikia pasipoti mpya.
  “Nipo nyumbani kushughulikiwa pasipoti mpya, natarajiwa kufanikisha mpango huu ndani ya siku mbili hizi na nikiipata mara moja narejea Lubumbashi,”amesema Ulimwengu. 
  Jumamosi wenyeji walitangulia kwa bao la kiungo Hamza Lahmar dakika ya 20, kabla ya Rogger Assale kuisawazishia Mazembe dakika ya 52.
  Mazembe sasa watahitaji hata sare ya 0-0 katika mchezo wa marudiano nyumbani Septemba 25 mjini Lubumbashi ili kwenda fainali, ambako watakutana na mshindi wa jumla kati ya Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria na FUS Rabat ya Morocco.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU: NATAKA KUBEBA KOMBE LA SHIRIKISHO PIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top