• HABARI MPYA

    Tuesday, May 10, 2016

    YANGA 71 TASLIMU, MBEYA CITY AFA 2-0 SOKOINE

    Na David Nyembe, MBEYA
    YANGA imezidi kuupendezesha ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Yanga sasa inafikisha pointi 71, baada ya kucheza mechi 28 na ikiwa imebakiza mechi mbili dhidi ya Ndanda FC na Majimaji kukamilisha msimu.
    Hadi mapumziko, tayari Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na beki Mtogo, Vincent Bossou.
    Bossou alifunga bao hilo kwa kichwa dakika ya 15, akimalizia krosi ya beki mwenzake, Juma Abdul kutoka kulia aliyeanzishiwa kona fupi na winga Simon Msuva.
    Amissi Tambwe akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la pili
    Beki Mtogo wa Yanga akikimbia kushangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza leo

    Hata hivyo, Yanga ilipoteza wachezaji wake wawili kipindi cha kwanza, mfungaji wa bao Bossou na kiungo Mkongo Mbuyu Twite ambao wote waliumia.
    Nafasi ya Twite ilichukuliwa na Salum Telela dakika ya nane na Kevin Yondan alichukua nafasi ya Bossou dakika ya 29.
    Kwa ujumla Yanga ilitawala mchezo kipindi cha kwanza na ingeweza kuondoka inaongoza kwa mabao zaidi kama si kosakosa za wazi mbili tatu.
    Kipindi cha pili, nyota ya wana Jangwani iliendelea kung’ara na kuzidi kuwafunika wenyeji Mbeya City uwanjani.
    Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe akafunga bao lake la 21 katika Ligi Kuu msimu huu kuipatia Yanga bao la pili dakika ya 84 kwa shuti la nje kla 18.
    Mshambuliaji wa Zimbabwe, Donald Ngoma hakuwa mwenye bahati leo kutokana na kukosa mabao mawili ya wazi, moja kila kipindi wakati Simon Msuva alipoteza nafasi moja nzuri kipindi cha pili. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk80.
    Mbeya City; Juma Kaseja, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Tumba Swedi, Haruna Shamte, Kenny Ally, Suleiman Mangoma/Hamidu Mohamed dk66, Ramadhani Chombo ‘Redondo/Raphael Alpha dk46, Salvatory Nkulula, Geoffrey Mlawa na Joseph Mahundi/Ditram Nchimbi dk76.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA 71 TASLIMU, MBEYA CITY AFA 2-0 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top