• HABARI MPYA

  Monday, May 09, 2016

  RADIO ONE NA HADHITHI YA MAITI KUPIGA CHAFYA

  NILIWAHI kusoma kisa moja cha kusisimua cha mtu aliyedhaniwa kufariki, ‘kufufuka’ akiwa kishaingizwa kaburini tayari kwa kuzikwa.
  Kisa hicho kikasema kuwa wakati mwili ukiwa umeshawekwa kaburini, ndipo mtu huyo akapiga chafya na kuwafanya watu waliokuwa mazishini kutaharuki na wengine kukimbia bila hata kugeuka nyuma. Lakini wapo pia walioshukuru na kufarijika kuwa mpendwa wao bado yuko hai. 
  Kufuatia tukio hilo, wako waliaomini kuwa mtu yule hakuwa amefariki bali alikuwa amerizai na pengine ni upeo mdogo wa utambuzi wa mambo ndiyo uliopelekea ndugu na jamaa waamini kuwa mpendwa wao amefariki na wakaandaa taratibu zote za mazishi.

  Wako pia waliomini kuwa ule ulikuwa ni muujiza na kwamba mtu yule alifariki kweli na akafufukia makaburini. Ili mradi kila mtu alisema lake.
  Kisa hiki nakifananisha na soko la muziki wa dansi hapa nchini ambapo wako wanaodhani muziki huo umekufa na wako wanaomini kuwa umezirai, ingawa wapo pia wachache wanaoamini kwamba muziki wa dansi bado uko juu.
  Vyombo vingi vya habari hususan radio na televisheni, vimeutupa muziki wa dansi, hali inayofanya bendi nyingi zijiulize kama kweli kuna haja ya kurekodi nyimbo mpya. Unarekodi nyimbo mpya ili zipigwe wapi? Hilo ndilo swali wanaolojiuliza wamiliki wengi wa bendi za dansi.
  Zipo sababu nyingi zinazotolewa na vituo vya radio na televisheni juu ya ukame wa muziki wa dansi kwenye vyombo hivyo muhimu vya habari. Tungo mbovu, nyimbo ndefu, kiwango cha hali ya chini cha utengenezaji wa nyimbo na video, ni baadhi tu ya sababu zinazotolewa na wahusika wengi wa vituo vya redio na televisheni.
  Baadhi ya sababu ni za ukweli lakini ni kwa baadhi ya nyimbo, kwa baadhi ya bendi na kwa baadhi ya wasaanii, lakini kusema kuwa hakuna kabisa nyimbo nzuri, tungo nzuri, video nzuri ni UONEVU.
  Kwa hali hiyo basi, niletegemea angalau hizo kazi chache nzuri, zingepata muda wa kuchanua kwenye vituo vya radio na televisheni lakini badala yake imekuwa hadithi ya samaki akioza NI WOTE WAMEOZA.
  Napenda nichukue fursa hii kuipongeza Radio One Stereo kwa kuanzisha kipindi kipya cha muziki wa dansi kilichopewa jina la AFRO TZ kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Alhamisi kuanzia saa 4 usiku hadi 7 usiku. Mungu awepe nini tena wasanii wa muziki wa dansi.
  Radio One ni kama imekuja kuuzindua upya muziki wa dansi ambao labda umezirai kama si kufa. Imefanya muziki wa dansi upige chafya ukiwa ndani ya chumba cha wagonjwa mahututi kama si chumba cha kuhifadhia maiti.
  Ni wazi sasa bendi zetu zitaanza kurekodi kwa wingi kazi mpya maana sasa wana uwanja mpana wa kwenda kunadi kazi zao, ni wazi pia kuwa jambo kama hili kufanywa na radio kubwa kama Radio One, basi vituo vingi vya radio vitaiga hatua hiyo na huo utakuwa ni ukombozi wa muziki wa dansi.
  Ni nini tofauti ya Afro TZ na vipindi vingine vya radio vinavyoamini kuwa vinapiga muziki wa dansi? Tofauti ni kwamba Afro TZ inapiga muziki wa dansi wa Tanzania peke yake, wakati vipindi vingine vingi vinapiga muziki wa Kifarika - muziki wa kutoka kila pembe ya Afrika na hivyo kuuweka ‘mtu kati’ muziki wa dansi kwenye vipindi hivyo vingine.
  Katika utitiri wa vituo vya radio vilivyosambaa kote nchini, unaweza ukatafuta kwa darubini aina ya vipindi kama Afro TZ na usivione.
  Hongera sana Radio One, hongera mtangazaji wa kipindi cha Afro TZ Rajab Zomboko, hongera Mkurugenzi wa Radio One, Deo Rweyunga, hongera Mkurugenzi Mtendaji wa Radio One na ITV, Bibi Joyce Mhaville na hongera pia kwa mwenyekiti wa IPP Reginald Mengi kwa uamuzi huo utakaokoa kazi na maisha ya kisanii ya wanamuziki wa dansi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RADIO ONE NA HADHITHI YA MAITI KUPIGA CHAFYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top