• HABARI MPYA

  Wednesday, April 13, 2016

  YANGA NA AZAM ZAPINGA RATIBA KOMBE LA ASFC

  Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
  YANGA SC na Azam zote zimekataa kucheza Nusu Fainali ya Kombe Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federations Cup (ASFC) 2016 Aprili 24.
  itamenyana na Coastal Union katika Nusu Fainali ya michuano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federations Cup 2016.
  Yanga watakuwa wageni wa Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga Aprili 24, mwaka huu, siku ambayo Azam FC itamenyana na Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga. 
  Hiyo inafuatia droo iliyopangwa jana studio za Azam TV, wadhamini wa michuano hiyo, Tabata, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa.
  Zote zimekuja na sababu sawa, kwamba zitakuwa na mechi za michuano ya Afrika Aprili 20 ugenini na zinatarajia kurejea Dar es Salaam Aprili 21 usiku, hivyo watakuwa na muda mfupi kabla ya mechi za Kombe la TFF ambazo watacheza ugenini.
  Meneja wa Kitengo cha Michezo cha Azam TV, Baruwan Muhuza akiwa ameshika Kombe la ASFC wakati wa droo

  Yanga watakuwa wageni wa Al Ahly mjini Alexandria Aprili 20, katika mchezo a marudiano hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrikaa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam Jumamosi.
  Na Azam FC watakuwa wageni wa Esperance mjini Tunis siku hiyo hiyo, katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika baada ya Jumapili kushinda 2-1 Dar es Salaam.
  Akizungumza baada ya upangwaji wa droo ya Nusu Fainali ya michuano hiyo studio za Azam TV usiku wa jana, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema kwamba ratiba imekaa vibaya.
  “Sisi tutacheza mechi Tunisia tarehe ya 20, ina maana kuondoka kule ni tarehe 21, tufike saa ngapi Dar es Salaam na saa ngapi tupate ndege ya kwenda Mwadui?”alihoji Kawemba.
  Wadau mbalimbali waliokuwepo wakati wa upangwaji wa droo hiyo wakifuatilia kwa makini
  Mmoja wa viongozi wa Azam TV, Charles Hillary akifuatilia zoezi hilo kishupavu

  Ameishauri TFF kuangalia uwezekano wa kusogeza mbele mechi hizo, ili kila timu ipate fursa ya kujiandaa vizuri.
  Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro naye alisema kwamba watacheza mechi Misri Aprili 20 na wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam Aprili 21, wakati Tanga njia kuu ni basi.
  “Ufike Dar es Salaam tarehe 21, uondoke kwa basi Dar es Salaam tarehe 22 kwenda Tanga kwa safari ya karibu nusu siku, kisha tarehe 24 ucheze mechi, hii ni ngumu sana,”alisema Muro.
  Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliyekuwapo kwenye droo hiyo aliwakatisha tamaa viongozi hao wa Yanga na Azam kwa kusema kwmaba hawaoni tatizo katika tarehe za Nusu Fainali. 
  Coastal Union iliingia Nusu Fainali baada ya kuitoa Simba SC kwa kuifunga mabao 2-1, wakati Azam FC iliitoa Prisons kwa kuifunga 3-1, Mwadui FC iliitoa Geita Gold kwa kufunga 3-0 na Yanga SC iliwafunga Ndanda FC 2-1.
  Bingwa wa Kombe la ASFC, michuano iliyoanza na timu 64 Novemba mwaka jana, ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
  Katika hatua ya awali, kila timu ilipatiwa fedha za usafiri Sh Milioni 3, na vifaa vya mashindano kutoka kwa wadhamini, Azam TV ikiwa ni sehemu ya udhamini wa Bilioni 3.3, wakati bingwa atajinyakuliwa kitita cha Sh. Milioni 50,
  Fainali inatarajiwa kuchezwa wiki moja baada ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kumalizika.
  Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu ikaifunga Baker Rangers ya Magomeni katika fainali, wakati ikijulikana kama Kombe la FAT (Chama cha Soka Tanzania).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NA AZAM ZAPINGA RATIBA KOMBE LA ASFC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top