• HABARI MPYA

  Saturday, April 09, 2016

  YANGA NA AL AHLY TAIFA LEO MARUDIO YA PAMBANO LA 2014, MUENDELEZO WA VITA ILIYOANZA 1982

  REKODI YA YANGA NA AL AHLY
  Ligi ya Mabingwa Afrika; 1982
  RAUNDI YA PILI:
  Al- Ahly 5-0 Yanga (Misri) 
  Yanga SC 1-1 Al- Ahly (Dar) 
  Ligi ya Mabingwa; 1988
  RAUNDI YA KWANZA:
  Yanga 0-0 Al-Ahly (Dar)
  Al- Ahly 4-0 Yanga (Misri) 
  Ligi ya Mabingwa; 2009
  RAUNDI YA KWANZA
  Al Ahly 3-0 Yanga (Misri)
  Yanga 0-1 Al Ahly (Dar)
  Ligi ya Mabingwa; 2014
  RAUNDI YA KWANZA
  Yanga SC 1-0 Al Ahly (Dar)
  Al Ahly 1-0 Yanga SC (Misri)
  (Yanga ilitolewa kwa penalti 4-3)
  Haruna Niyonzima wa Yanga akipambana na kiungo wa Al Ahly mwaka 2014 Uwanja wa Taifa. Niyonzima hatakuwepo leo kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga SC leo wanatupa kete yao ya kwanza katika hatua ya 16 Bora watakapomenyana na Al Ahly ya Misri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga imerejea jana jioni Dar es Salaam kutoka kisiwani Pemba ilikokuwa imeweka kambi ya takriban wiki moja katika hoteli ya Misali Sun Set Beach, Chake Chake kujiandaa na mchezo huo.
  Wapinzani wao, Ahly wapo Dar e Salaam tangu Jumatano, wakiwa wameweka kambi katika hoteli ya Serena, wakifanya mazoezi Uwanja wa Gymkhana, kabla ya jana kuhamia Uwanja wa Taifa.
  Mchezo huo umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini, hususan wa Yanga yenyewe kutokana na historia ya timu hizo zinapokutana. 
  Hii inakuwa mara ya tano, Yanga kukutana na Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mara zote nne za awali timu ya Jangwani, Dar es Salaam ikitolewa. 
  Mara ya kwanza wababe hao walikutana mwaka 1982 katika Raundi ya Pili na Yanga ikatolewa kwa jumla ya 6-1 ikifungwa 5-0 Cairo na kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Mwaka 1988 zikakutana katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa jumla ya mabao 4-0 waliyofungwa Cairo baada ya kutoka sare ya 0-0 Dar es Salaam.
  Mwaka 2009 Yanga wakatolewa kwa jumla ya mabao 4-0 wakifungwa 3-0 Cairo na 1-0 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza pia.
  Yanga ikaandika historia mwaka 2014 ilipowafunga kwa mara ya kwanza Al Ahly Dar es Salaam 1-0, bao pekee la Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kabla ya kwenda kufungwa 1-0 mjini Alexandria.
  Mchezo ukarefushwa hadi dakika 120 kabla ya Ahly kushinda kwa penalti 4-3.
  kwa ujumla, Yanga haijawahi kuitoa timu yoyote ya Kaskazini mwa Afrika kwenye michuano ya Afrika na Al Ahly inakuwa timu pekee ya huko kuwahi kufungwa na mabingwa hao wa Tanzania.
  Mwaka 1992, Yanga ilitolewa na Ismailia ya Misri katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa, ikifungwa 2-0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kulazimisha sare ya 1-1 Cairo.
  Mwaka 1998 Yanga ilifungwa 6-0 na Raja Casablanca ya Morocco katika mchezo wa Kundi B Ligi ya Mabingwa kabla ya kutoa sare ya 3-3 mchezo wa marudiano Dar es Salaam.
  Mwaka 2000 Yanga ililazimishwa sare ya 1-1 na Zamalek ya Misri mjini Dar es Salaam katika iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi kabla ya kwenda kufungwa 4-0 Cairo katika Raundi ya Kwanza.
  Mwaka 2007 Yanga ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutoa sare 0-0 Mwanza.
  Yanga iliingia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kutolewa na El Merreikh ya Sudan, ikitoa sare ya 0-0 Mwanza na kufungwa 2-0 Khartoum.
  Mwaka 2008 Yanga ilifungwa 1-0 na Al Akhdar ya Libya mjini Tripoli kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika. 
  Mwaka 2012 Yanga ililazimisha sare ya 1-1 na Zamalek ya Misri mjini Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 mjini Cairo.
  Yanga inakutana na Ahly leo ikitoka kuzitoa Cercle de Joachim ya Maurtius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 2-1 ugenini na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Al Ahly ilianzia Raundi ya Kwanza na kuitoa Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 0-0 ugenini kabla ya ushindi huo nyumbani.
  Zote, Ahly na Yanga zimeshinda mechi nne nne na sare moja moja katika mechi tano tano zilizopita na zimeshinda mechi zote za mashindano ya nyumbani. 
  Mara ya mwisho Yanga ilifungwa Januari 30, mwaka huu na Coastal Union 2-0 katika Ligi Kuu ugenini, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wakati Ahly ilifungwa mara ya mwisho Desemba 17, mwaka jana 3-0 nyumbani na Smouha katika Ligi Kuu ya Misri.
  Zote zimeshinda 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa jadi hivi karibuni, Ahly wakiifunga Zamalek Februari 9 mabao ya Malick Evouna dakika ya 56 na Amr Gamal dakika ya 89, Yanga wakiifunga Simba Februari 20, mabao ya Donald Dombo Ngoma dakika ya 39 na Amissi Joselyn Tambwe dakika ya 72.
  Zote zinafundishwa na makocha Waholanzi, Yanga ikiwa na Hans van der Pluijm mwenye umri wa miaka 67 na Ahly ikiwa na Maarten Cornelis Jol maarufu kama Martin Jol, mwenye umri wa miaka 60.
  Al Ahly inaongoza Ligi ya Misri ikiwa na pointi 50 za mechi 22, wakati Yanga yenye pointi 53 za mechi 22 ni ya pili katika Ligi ya Tanzania.
  Je, nani atashangilia ushindi baada ya dakika 90 leo Uwanja wa Taifa, ni Yanga au Ahly?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NA AL AHLY TAIFA LEO MARUDIO YA PAMBANO LA 2014, MUENDELEZO WA VITA ILIYOANZA 1982 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top