• HABARI MPYA

    Thursday, April 07, 2016

    MWESIGWA ARUKA 'FUTI 600' KUHUSIKA NA NJAMA CHAFU TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine amekanusha kuhusika na njama za upangaji matokeo ya michezo ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
    Na Mwesigwa ametishia kulifikisha mahakamani gazeti moja la kila siku nchini lililochapisha habari za kumuhusisha na mpango huo mchafu. 
    "Nimeshitushwa na kusikitishwa sana na habari hiyo juu yangu ambayo ni ya kutunga, yenye nia mbaya isiyokuwa ukweli wowote, kwani sijawahi kukaa na watu wowote kupanga njama yoyote iliyo kinyume na maadili ya mchezo wa mpira wa miguu,"amesema Mwesigwa.
    Selestine Mwesigwa (kulia) akiwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi

    Gazeti moja la leo nchini, limechapisha habari katika ukurasa wake wa 24 chini ya kichwa cha habari " Vigogo TFF wajikaanga" likisema katika ibara ya 7 kuwa kwenye mazungumzo yaliyochukua zaidi ya dakika 10 yalimhusisha pia Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa.
    Hamkani si shwati TFF, baada ya kuvuja kwa sauti za maofisa wa shirikisho hilo wakiomba rushwa ya Sh. Milioni kutoka kwa viongozi wa timu moja ya Daraja la Kwanza ili waisaidie kupanda Ligi Kuu.
    Na jana TFF imetoa tamko la kusikitishwa na taarifa hizo na kuahidi kuwachukuliwa hatua kali maofisa wake waliohusika, ingawa imesema taarifa hizo hazihusiani na kesi ya kupanga matokeo iliyoamuliwa Aprili 3.
    TFF imesema kwanza inachunguza kubaini uhalisia (authenticity) wa taarifa hizo na itachukua hatua kali sana kwa watumishi wa shirikisho na viongozi wa timu husika watakaobainika kushiriki vitendo vilivyo kinyume na maadili ya mpira wa miguu.
    Tayari Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano TFF, Martin Chacha, mmoja wa watuhumiwa ameacha kazi tangu juzi.
    Katika barua yake aliyomwandikia Katibu Mkuu wa TFF, Chacha amesema amepata majukumu mapya ya kikazi ambayo pamoja na majukumu ya kifamilia yatamfanya akose muda wa kutumika vema katika nafasi yake katika Shirikisho
    Chacha alijiunga na TFF Julai 2014 kama Ofisa Mashindano na baadaye kuteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano, kufuatia aliyekuwa anashikiria nafasi hiyo Boniface Wambura kuteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWESIGWA ARUKA 'FUTI 600' KUHUSIKA NA NJAMA CHAFU TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top