• HABARI MPYA

  Monday, April 11, 2016

  MCAMEROON WA YANGA AWATUPA NJE SIMBA KOMBE LA SHIRIKISHO

  Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
  NDOTO za Simba SC kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani zimyeyuka kwa asilimia kubwa leo, baada ya kutolewa na Coastal Union katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup leo.
  Hiyo ni baada ya kufungwa mabao 2-1 na Coastal Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao yote ya Wagosi wa Kaya yakifungwa na mshambuliaji kutoka Cameroon Youssouf Sabo aliyewahi kufanya majaribio Yanga, yote kwa mipira ya adhabu. 
  Sabo, aliyetokea Cotton Sport ya kwao, alianza kuifungia Coastal Union dakika ya 19 kwa shuti la mpira wa adhabu umbali wa mita zaidi ya 20 na kutinga nyavuni moja kwa moja likimpita kipa Muivory Coast, Vincent Angban.
  Wachezaji wa Coastal wakimpongeza Youssouf Sabo baada ya kufunga bao la pili

  Kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Hamisi Kiiza akatokea benchi kipindi cha pili na kwenda kuisawazishia Simba bao hilo.
  Ilimchukua dakika mbili tu uwanjani Kiiza kuisawazishia Simba baada ya kuingia dakika ya 47 kuchukua nafasi ya kiungo wa Zimbabwe, Justice Majabvi.
  Hata hivyo, Sabo tena akaifungia Coastal bao la ushindi kwa penalti dakika ya 85, kufuatia beki Novaty Lufunga kumuangusha kwenye boksi mshambuliaji Ally Ahmed ‘Shiboli’.
  Mshambuliaji wa Simba, Paul Kiongera akimtoka beki wa Coastal Union, Hamad Juma
  Kiungo Awadh Juma akimbembeleza Nahodha Mussa Mgosi baada ya mchezo
  Sabo (kulia) alipokuwa Yanga kwa majaribio mwaka jana kabla ya kwenda Coastal Union

  Refa Alex Mahagi wa Mwanza pamoja na kutenga tuta akamtoa kwa kadi nyekundu Lufunga na kuidhoofisha kabisa Simba. 
  Kwa ushindi huo, Coastal inaungana na  Azam FC, Mwadui FC, na Yanga SC kukata tiketi ya kucheza Nusu Fainali.
  Droo ya Nusu Fainali inatarajiwa kufanyika kesho Saa 3:00 usiku moja kwa moja kupitia chaneli ya Azam Two ya Azam TV.
  Robo nyingine za michuano hiyo iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana kwa kushirikisha timu 64, Azam FC iliitoa Prisons kwa kuifunga 3-1, Mwadui FC iliitoa Geita Gold kwa kufunga 3-0 na Yanga SC iliwafunga Ndanda FC 2-1.
  Ikumbukwe bingwa wa Kombe la ASFC ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
  Kikosi cha Simba kilikuwa; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Novaty  Lufungo, Justice Majabvi/Hamisi Kiiza dk47, Hassan Kessy, Jonas Mkude, Danny Lyanga, Ibrahim Hajibu na Said Ndemla/Awadh juma dk46.
  Coastal Union; Fikirini Bakari, Said Jeilan/Ally Ahmed ‘Shiboli’ dk46, Mbwana Hamisi ‘Kibacha’, Abdulhahlim Humud, Twaha Ibrahim ‘Messi’, Godfrey Wambura, Juma Mahadhi na Tumaini Mosha.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MCAMEROON WA YANGA AWATUPA NJE SIMBA KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top