• HABARI MPYA

  Tuesday, April 19, 2016

  AZAM FC HATARINI KUMKOSA FARID MUSSA MCHEZO WA MARUDIANO NA ESPERANCE

  Na Princess Asia, TUNIS
  KOCHA Muingereza wa Azam FC, Stewart John Hall amesema kwamba hana uhakika wa kumtumia winga wake machachari, Farid Mussa katika mchezo dhidi ya Esperance usiku wa Jumanne.
  Farid aliumia katika mazoezi ya Jumapili jioni mjini hapa baada ya kugongana na beki Said Mourad na kwa bahati mbaya, akagongana na beki huyo huyo katika mazoezi ya siku iliyofuata na kujitonesha maumivu.
  “Jana amegongwa na Mourad, na leo tena amegongwa na yule yule Mourad, sasa sina uhakika wa kumtumia. Kwa sasa yupo chini ya uangalizi wa Daktari. Nitajua kesho,”amesema Hall akimaanisha atajua siku ya mchezo wenyewe.
  Farid Mussa (kulia) akimlamba chenga Said Mourad kabla ya kugongana naye na kuumia kwenye mazoezi ya Jumatatu usiku


  Azam FC Jumapili imefanya mazoezi yake ya kwanza Uwanja wa hoteli ya Carthage Thalasso na Jumatatu ikafanya kwenye Uwanja wa Olimpiki Novemba 7 mjini Rades, Tunis ambao utatumika kwa mchezo huo.
  Katika mchezo huo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC inahitaji sare ili kusonga mbele baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
  Na Farid Mussa alifunga bao la kwanza kabla ya kumsetia Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyefunga la pili Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam ikitoka nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 2-1 nyumbani.
  Tayari Azam FC itawakosa wachezaji wake wanne wa kikosi cha kwanza, mabeki Shomary Kapombe, ambaye ni mgonjwa, Serge Wawa majeruhi, kiungo Jean Baptiste Mugiraneza anayetumikia adhabu ya kadi na mshambuliaji Kipre Herman Tchetche majeruhi pia.  
  Kapombe alikosa mchezo wa kwanza pia Dar es Salaam, wakati Wawa aliumia dakika za mwishoni kwenye mchezo wa kwanza na Esperance na Kipre aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa.
  Iwapo itashinda, Azam itaingia kwenye kapu la mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, ikimenyana na moja ya timu nane zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC HATARINI KUMKOSA FARID MUSSA MCHEZO WA MARUDIANO NA ESPERANCE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top