• HABARI MPYA

    Sunday, March 20, 2016

    YANGA WAMEONA FAIDA YA DHARAU

    WAHENGA walisema; “Mdharau mwiba, mguu humuota tende”.
    Usemi huo bado kidogo utimie jan kwa Yanga baada ya kunusurika kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na APR ya Rwanda, licha ya kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza ugenini.
    Yanga SC imefanikiwa kwenda hatua ya 16 Bora michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.

    Yanga SC jana ililazimishwa sare ya 1-1 na timu ya jeshi la Rwanda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam – na kwa kuwa ilishinda 2-1 katika mchezo wa kwanza mjini Kigali wiki iliyopita, imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2.
    Yanga sasa watamenyana na Al Ahly ya Misri ambayo imeitoa Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ushindi iliyoupata mjini Cairo jana baada ya sare ya 0-0 Angola wiki iliyopita. 
    Katika mchezo wa jana, APR ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tatu kupitia kwa Fiston Nkinzingabo aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Jean Claude Iranzi.
    Yanga walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 28 kupitia kwa mshambuliaji wake, Donald Dombo Ngoma aliyefumua shuti la kitaalamu baada ya pasi nzuri ya kiungo Mzimbabwe mwenzake, Thabani Scara Kamusoko.
    Baada ya mchezo kuwa 1-1, kama APR wangepata bao hata dakika ya mwisho, ina maana kila timu ingekuwa imeshinda 2-1 ugenini na hiyo kuwa sare na mechi hiyo ingekwenda hadi kwenye mikwaju ya penalti.
    Inafahamika Yanga ina ugonjwa wa asili wa kutetemekea mikwaju ya penalti, kwani inapofikia hatua hiyo wenyewe hujikatia tamaa mapema.
    Ni mara chache mno Yanga imeweza kufuzu au kushinda katika mikwaju ya penalti – na ndiyo maana ninasema jana wamenusurika.
    Na haya ni matunda ya kudharau mechi, kwani baada ya ushindi wa 2-1 mjini Kigali, Yanga waliona kama tayari wamemaliza kazi na hawakuona haja ya maandalizi mazuri kwa mchezo wa marudiano.
    Waliweka kambi uswahilini Kariakoo ambako ni eneo la makazi ya watu, lenye pilika nyingi usiku na mchana na lipo karibu na barabara kubwa ya Morogoro, ambako gari zinapita saa 24 kwa kasi ya kuvuma, miungurumo na honi nyingi.
    Wazi wachezaji hawakupata utulivu uliostahili katika kambi ile waliyowekwa kuelekea mchezo wa marudiano na APR na matokeo ya jana ni matunda ya viongozi kutoupa uzito wake mchezo huo.
    Leo tumshukuru Mungu kwa pamoja, Yanga wamefuzu – lakini kama wangetolewa ingekuwa habari nyingine.
    Kwanza moto ungewawakia viongozi kutoka kwa mashabiki wao wenyewe na pili wangevurugana katika kipindi hiki ambacho wanahitaji utulivu ili kuweza kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam na Simba zenye nafasi ya kuutwaa pia.
    Kilichofanywa na Yanga kuelekea mchezo wa marudiano na APR hakina tafsiri nyingine zaidi ya dharau, ambayo haipaswi kurudiwa.
    Kulaumiana kumepitwa na wakati, bali siku hizi kuna kupeana ukweli na kuukubali, ili kujifunza kutokana na makosa.
    Na umefika wakati kweli viongozi wa Yanga wawe wanajifunza kutokana na makosa ili waonyeshe kweli wao ni watu wa mpira na wanaujua mpira.
    Sasa wanakwenda kukutana na wababe wao wa kihistoria, Al Ahly ya Misri katika mchezo mgumu zaidi, huku wengi miongoni mwa Watanzania hususan watani wao, Simba wakiamini safari imefikia mwisho.
    Yanga wamekutana na Ahly mara kibao na mara zote wametolewa, ingawa mara ya mwisho walitolewa kwa mbinde.
    Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2014 katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa penalti 4-3, baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Mechi ya kwanza baina yaYanga na Al AHly itachezwa Aprili 9, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati marudiano yatakuwa Aprili 19 mjini Cairo.
    Ni wakati sasa viongozi wa Yanga na kocha Hans van der Pluijm ambaye alikuwepoo kazini mwaka juzi, wakati timu hiyo inatolewa na Ahly warudishe kumbukumbu zao nyuma na kujiuliza walikosea wapi. 
    Lakini niwaulize tu Yanga, jana wangesema nini kama wangetolewa baada ya uzembe walioufanya? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAMEONA FAIDA YA DHARAU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top