• HABARI MPYA

  Monday, March 14, 2016

  TWANGA PEPETA, DOUBLE M MSIJE NA MVINYO WA ZAMANI KWENYE CHUPA MPYA

  Ni lini umewahi kusikia bendi ya muziki wa dansi imeenda kuweka kambi ya miezi miwili nje ya nchi? Binafsi sikumbuki kama nimewahi kusikia hiyo kitu hapo kabla, ukiondoa tukio la hivi karibuni la bendi ya Double M Plus.
  Bendi hiyo inayoongozwa na Mwinjuma Muumin iliweka kambi nchini Msumbiji baada ya kuwanyakua wanamuziki wapya wenye majina makubwa kama vile Saleh Kupaza na Dogo Rama kutoka Twanga Pepeta.
  Ilikuwa ni kambi ya kupika vitu vipya iliyozaa nyimbo mpya tatu ambazo tayari zimeshaingizwa studio: “Ganda la Muwa”, “Mapungufu Yangu” na “Siri ya Mgongo”.

  Matokeo ya kambi hiyo ya Msumbiji yanategemewa kuonekana Ijumaa hii ndani ya ukumbi wa Mango Garden Kinondoni wakati bendi hiyo itakapotambulishwa rasmi sambamba na nyimbo zao mpya na wasanii wapya.
  Double M Plus ni jina lililokarabatiwa kutoka iliyokuwa Double M Sound, moja ya bendi iliyowahi kutingisha kwenye soko la muziki wa dansi kwa vipindi tofauti tofauti – ikiibuka na kupotea.
  Chini ya jina jipya, wasanii wapya, nyimbo mpya na kambi nje ya nchi, bendi hii inasubiriwa kwa hamu huku mashabiki wengi wakitaraji makubwa kutoka kwao.
  Lakini Double M Plus inapaswa kujua kuwa muziki umebadilika, soko limekuwa gumu na sasa mashabiki wachache wanaojitokeza kwenda kwenye kumbi za burudani wanahitaji kitu kipya, ladha mpya na ubunifu mpya vinginevyo idadi yao itazidi kupungua badala ya kuongezeka.
  Double M Plus inapaswa kutambua kuwa jukumu lake la kwanza ni kupora mashabiki wa bendi zingine kabla haijazalisha mashabiki wapya, hivyo basi ni lazima wawe na kitu tofauti kilichojaa kila aina ya ubora utakaokuwa chachu ya kupora mashabiki hao kutoka katika bendi wanazozishabikia.
  Ukiachana na Double M Plus, Jumamosi ya tarehe 19 (siku moja baada ya onyesho la Double M) kutakuwa na onyesho maalum la Twanga Pepeta hapo hapo Mango Garden.
  Twanga Pepeta wanakuja na kauli mbiu ya “Twanga 18” wakimaanisha wanasherehekea mwaka wao wa 18 huku wakiwa na ujio wa rapa aliyerudishwa kundini Saulo Jonh “Ferguson”.
  Bendi hiyo itakuwa inatokea Dodoma ilipoweka kambi ya wiki mbili. Sikumbuki  katika miaka ya hivi karibuni ni lini Twanga Pepeta walisimamisha maonyesho yao na kwenda kuweka kambi nje ya jiji la Dar es Salaam. 
  Lakini wito wangu kwa Twanga Pepeta ni kama ule ule nilioutoa kwa Double M Plus – watu wanataka mambo mapya. Masuala ya kupiga wimbo mmoja jukwaani kwa dakika 25 au 30 hayana mpango, vituko vya waimbaji kushindana kutaja majina ya madeshee ukumbini ili wakapande jukwaani na kutunza pesa, kunapoteza ladha. 
  Yaani inafika wakati mwimbaji anasema: “Fulani sijakuzoea hivyo” kisa? Eti kwasababu hajapeleka mshiko jukwaani.
  Soko linahitaji wasanii nadhifu jukwaani, muziki usioumiza masikio, tungo maridadi na zinazoeleweka kiurahisi, mpangilio mzuri wa ala na uimbaji, nyimbo fupi zisizochusha na kubwa zaidi ni nidhamu ya uwajibikaji kwa wasanii jukwaani.
  Twanga Pepeta na Double M Plus  msipokuja na mabadiliko kwenye nyimbo na maonyesho yenu kambi zenu mlizoweka zitakuwa ni sawa na majipu yanayostahili kutumbuliwa - hamtakuwa na tofauti yoyote ya ile hadithi ya mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TWANGA PEPETA, DOUBLE M MSIJE NA MVINYO WA ZAMANI KWENYE CHUPA MPYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top