• HABARI MPYA

  Sunday, March 20, 2016

  “TUDO DE BOM” AZAM FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WARENO wanasema “Tudo de Bom”, yaani kila la heri, hivyo unavyoweza kusema kwa wawakilishi wetu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, Azam FC.
  Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC leo watakuwa wenyeji wa Bidvest Wits ya Afrika Kusini katika mechi ya marudiano Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Azam wanapewa nafasi kubwa ya kutinga raundi ya pili ya michuano hiyo baada ya kushinda 3-0 katika mechi ya kwanza jijini Johannesburg, Afrika Kusini wiki iliyopita.
  Washambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche na Allan Wanga leo wanatarajiwa kuisaidia timu yao Chamazi

  Wanalambalamba waliuanza msimu wa 2015/16 kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame bila kupoteza hata mechi moja, lakini wakatokewa mapema Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar kabla ya kutwaa ubingwa mashindano maalum ya timu nne nchini Zambia.
  Kurejea kikosini mwa beki kisiki, Aggrey Morris aliyepona majeraha ya goti, kumekiimarisha zaidi kikosi cha Muingereza, Stewart Hall ambacho kinaendelea kutesa na washambuliaji Kipre Tchetche na John Bocco.
  Beki wa pembeni Shomari Kapombe ambaye alikuwa mmoja wa wafungaji katika mechi ya kwanza jijini Johannesburg, anazidi kung'ra kwa kutupia magoli muhimu msimu huu. Mchezaji huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa ametupia mara nane katika mechi 21 zilizopita za Ligi Kuu.
  Azam FC pia wanapewa nafasi kubwa ya kuwatungua tena Bidvest kutokana na mechi hiyo kuchezwa mchana jua kali (kuanzia saa 9:15 alasiri), muda ambao si rafiki kwa timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) ambayo nyota wake wamezoea baridi la 'Sauzi'.
  Mechi hiyo itachezeshwa na Gait Oting akisaidiwa na Abdallah Gassim na Casim Dehiya, huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Ariel James, wote kutoka Sudan Kusini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: “TUDO DE BOM” AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top