• HABARI MPYA

    Wednesday, March 16, 2016

    SIMBA YAWABADILIKIA ETOILE 'MPUNGA' WA OKWI

    Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imewaandikia barua Etoile du Sahel ya Tunisia kuomba nakala za nyaraka za malipo waliyofanya benki juu ya fedha za manunuzi ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi.
    Hatua hiyo inafuatia Simba kuona wanaendelea kuzungushwa juu ya malipo yao ya mauzo ya Okwi, licha ya agizo la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kutaka walipwe haraka.
    Simba ilimuuza Okwi ambaye sasa yuko Denmark akicheza soka la kulipwa kwa Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dau la Dola za Marekani 300,000 (sawa na Sh. milioni 600).
    Rais wa Simba, Evans Aveva amesema kwamba Etoile hawajatuma fedha za Okwi
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema hadi jana mchana hakuna fedha yoyote ambayo wamepokea na kuitaja Etoile du Sahel imewajibu kwa njia ya simu kwamba tayari wameshawekwa fedha kwenye akaunti ya klabu hiyo yenye makao makuu yake mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini.
    Aveva alisema kuwa baada ya kuona wanaendelea kuzungushwa, wamewaandikia barua viongozi wa klabu hiyo ya Tunisia ya kuwataka wawatumie nakala za nyaraka ambazo walipewa baada ya kuzituma fedha.
    "Bado tumeendelea kuzisikia tu hizo pesa kwa maneno, Etoile du Sahel walituambia kwa simu wameshatutumia lakini hii ni zaidi ya wiki ya pili hakuna tulichopokea, tumewaeleza wazitume nyaraka, kama hawatafanya hivyo, tutalikumbusha upya suala hili Fifa," alisema Aveva.
    Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kundi la Friends of Simba, aliongeza kuwa kuhusiana na fedha za mgawo wa mshambuliaji wao wa zamani, Mbwana Ally Samatta, nazo wanazisubiri kutoka TP Mazembe ambayo wenyewe wameonyesha nia ya kuwatumia mapema baada ya wao nao kukamilishiwa taratibu na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
    Alieleza kwamba mara baada ya kupata fedha hizo, wanatarajia kulipa baadhi ya madeni yanayowakabili na kiasi kingine kitaelekezwa kwenye programu za maendeleo za timu hiyo.
    "Tunahitaji fedha, kama zitakuja sasa zitatusaidia sana kukamilisha mipango ya maendeleo ya klabu, tunachokipata kwenye ligi ni kiasi kidogo hivyo mambo mengi yanakwama," Aveva alisema.
    Wakati huo huo Aveva alisema kwamba kikosi cha timu hiyo kitaondoka jijini kesho Alhamisi kuelekea Tanga kwa ajili ya mechi yake ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Coastal Union itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAWABADILIKIA ETOILE 'MPUNGA' WA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top