• HABARI MPYA

  Wednesday, March 16, 2016

  SIMBA LIGI YAO, YANGA NA AZAM NAO...

  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeendelea na utaratibu wa kupangua ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jana kutoa marekebisho madogo mengine ya ratiba ya ligi hiyo.
  Mabingwa watetezi, Yanga hawatacheza tena mechi nyingine yoyote mwezi huu. Mara ya mwisho Yanga walicheza Ligi Kuu Machi 8, wakiwafunga 5-0 ndugu zao African Sports ya Tanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na watakuwa na mechi ya ligi hiyo tena Aprili 2, dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja huo.
  Na hiyo mechi ya Aprili 2 ipo shakani, kwani kama Yanga watafuzu hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, watakuwa na mechi kati ya Aprili 8 na 10 dhidi ya Al Ahly ya Misri, wakianzia nyumbani Uwanja wa Taifa kabla ya kurudiana kati ya Aprili 19 na 20 mjini Cairo.

  Kwa kawaida Yanga hucheza mechi zake Jumamosi, maana yake mchezo wa kwanza na Ahly wanaweza kucheza Aprili 9 na kama wataamua kuomba muda wa maandalizi zaidi kabla ya mechi hiyo ngumu – maana yake mechi yao ya Ligi Kuu na Kagera inawezwa kuahirishwa pia.
  Kwa mujibu wa marekebisho ya Ratiba ya Ligi Kuu yaliyotolewa jana, Azam FC watacheza na Stand United leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wakati Simba SC watacheza na Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 
  Bodi ya Ligi imelazimika kufanya marekebisho ya Ratiba ya Ligi Kuu kupisha ratiba ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2017.
  Taifa Stars itakuwa na mchezo wa kufuzu AFCON Kundi G dhidi ya Chad mjini N’Djamena Machi 23, kabla ya timu hizo kurudiana Machi 28, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na baada ya mechi za mwishoni mwa wiki za michuano ya klabu barani, Afrika kundi la kwanza la wachezaji wa Stars linatarajiwa kuondoka Jumapili kuelekea Chad.
  Yanga SC baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR Jumamosi mjini Kigali, watarudiana na timu hiyo ya jeshi la Rwanda Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa.
  Na Azam FC baada ya kushinda 3-0 mjini Johannesburg, Afrika Kusini dhidi ya wenyeji Bidvest Wits katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika, watarudiana na timu hiyo Jumapili, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kuna wakati popote duniani, kwenye mashindano yoyote upanguaji wa ratiba huwa hauepukiki – kwa mfano hivi karibuni tumeshuhudia mechi kadhaa za Ligi Kuu ya England zikiahirishwa sababu ya michuano ya Kombe la FA.
  Kufuzu kwa timu za Arsenal, Everton, Chelsea, West Ham United, Watford na Crystal Palace katika hatua ya Robo Fainali za Kombe la FA England kulifanya timu zote ziahirishiwe mechi zao za Ligi Kuu.
  Ndiyo maana sasa hivi ukitazama msimamo wa Ligi Kuu ya England kuna zimecheza mechi 28 kama Everton, wakati nyingine zina mechi 29 na nyingine 30.
  Lakini jitihada za Chama cha Soka England kuhakikisha hakuwa na tofauti kubwa ya mechi za kucheza baina ya timu za Ligi Kuu zinaonekana na ndiyo maana timu zote zilizokuwa kwenye Kombe la FA wikiendi hii zinarudi uwanjani, ikiwemo Manchester United kumenyana na Manchester City Jumapili Uwanja wa Etihad.
  Ligi nzuri ni ile ambayo haitengenezi tofauti kubwa ya idadi za mechi za kucheza ili kutengeneza mazingira sawa ya ushindani baina ya timu.
  Wakati tukiamini hivyo, tunaona hali ni tofauti kwa Tanzania, kwani TFF imeshindwa kabisa kutengeneza uwiano sawa wa idadi za mechi kucheza.
  Wakati England mechi za Kombe la FA zikiingilia ratiba ya Ligi Kuu, nchini Tanzania mechi za michuano ya Shirikisho  la Soka nchini (CAF), zimepangua Ratiba ya Kuu.
  Yanga wanaocheza Ligi Kuu ya Mbingwa Afrika na Azam FC waliopo kwenye Kombe ya Shirikisho mechi zao zimekuwa zikiahirishwa ili kuzipa fursa ya kucheza michuano ya CAF.
  Hali hiyo imeleta tafrani upande wa pili, kwa mahasimu Simba SC kulalamika kwamba wanachezeshwa mechi mfululizo, wakati wapinzani wao Azam na Yanga wanalundikiwa viporo.
  Hofu ya Simba ni baadaye wapinzani wao kuja kupanga matokeo katika mechi zao za viporo na kuvuna pionti na mabao watakavyo.
  Simba wako sahihi na pia tunahofia hatari ya upangaji wa matokeo baadaye, iwapo Simba wataendelea kuvuna wastani mzuri wa pointi na kuzidi kujiimarisha kileleni. 
  Jumamosi Simba watacheza mechi ya tatu ndani ya siku nane, wakati Azam watakuwa wamecheza mechi moja na Yanga watakuwa hawajacheza mechi yoyote. Na Yanga hawatakuwa na mechi tena, labda hadi Aprili kutokana na kupisha mechi za timu ya taifa, Taifa Stars kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.
  Na baada ya mechi za mwishoni mwa wiki za michuano ya klabu barani, Afrika wachezaji wa Stars wanatarajiwa kukusanywa Jumapili kabla ya safari Jumanne kuelekea Chad.
  Na kama timu nyingine, hususan Simba iliyo katika mbio za ubingwa zitaendelea kuchezeshwa, maana yake tutakuwa na ligi mbili ndani ya ligi moja, jambo ambalo hakika si zuri. 
  Na ndiyo maana leo, nawarudia Bodi ya Ligi, Kamati ya Mashindano na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ujumla kuketi na kutafakari ha hali halisi, baada ya hapo waje na suluhisho kabla hili halijawa tatizo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA LIGI YAO, YANGA NA AZAM NAO... Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top