• HABARI MPYA

  Sunday, March 13, 2016

  MKWASA: MIMI SIJUI KAMA CANNAVARO AMEJIUZULU, AKIPONA NITAMUITA STARS

  Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba hana taarifa rasmi za kujiuzulu kwa aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' (pichani kushoto).
  Aidha, Mkwasa amesema kwamba hajamuita Cannavaro katika kikosi chake cha sasa kwa sababu ni majeruhi, ila ataendelea kumuhitaji atakapopona.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE juzi, Mkwasa, alisema kwamba Cannavaro bado ana nafasi ya kucheza kwenye timu hiyo na anauhitaji uzoefu wake wa kupambana katika mazingira mbalimbali.
  "Bado ninamuhitaji, ana msaada mkubwa kwenye timu, ninamuheshimu ni mchezaji mzuri na mwenye nidhamu, sina tatizo naye lolote," alisema Mkwasa.
  Aliongeza kwamba mabadiliko aliyoyafanya ya kumpa beji ya unahodha mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ni ya kawaida na hayatokani na chuki dhidi ya beki huyo.
  Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema hajui kama Cannavaro amejiuzulu 

  Alisema pia wapo wachezaji wengine  kama Aggrey Morris wa Azam FC na Andrew Vincent wa Mtibwa Sugar wana uwezo mzuri, lakini amewaacha kutokana na kuwa majeruhi lakini watakapokuwa 'fiti' atawaita.
  Taifa Stars inatarajia kuondoka nchini Machi 20 kuelekea Chad kuwavaa wenyeji wao na kurejeana Machi 28 hapa jijini katika mechi za Kundi G za mashindano ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika hapo mwakani.
  Januari mwaka huu, Mkwasa alimteua Samatta kuwa Nahodha mpya wa Taifa Stars na John Bocco akaendelea kuwa Nahodha Msaidizi, jambo ambalo lilionekana kumkera Cannavaro naye akatangaza kutochezea tena Taifa Stars.
  Cannavaro alisema ni vyema angeitwa na kocha huyo kuambiwa juu ya uamuzi huo, kabla kuliko kusikia kupitia vyombo vya habari.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKWASA: MIMI SIJUI KAMA CANNAVARO AMEJIUZULU, AKIPONA NITAMUITA STARS Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top