• HABARI MPYA

  Monday, March 14, 2016

  HAJIB AWEKA 'BONGE LA REKODI' SIMBA SC

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib (pichani kulia) ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda mara mbili tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Simba SC tangu kuanzishwa kwake Septemba mwaka jana. Hajib ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Januari wa vinara hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo inakuwa ya nne tangu kuanzishwa kwa mfumo huo, lengo likiwa ni kuongeza morali na kuwazawadia wachezaji wanaofanya vizuri.
  Mshindi hupatikana baada ya kura zinapigwa na wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba na soka la Tanzania kwa ujumla kupitia simu za mkononi ambao pia wamejiunga na huduma ya Simba News pamoja na kwenye mitandao rasmi ya kijamii ya Simba Facebook www.facebook.com/simbatanzania Twitter na Instagram @simbasctanzania.
  Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Rais wa Simba, Evans Aveva amesema; “Sisi kama uongozi wa klabu yetu ya Simba tunaamini katika kuwapa motisha wachezaji wetu kila iitwapo leo na hii ni katika kuongeza chachu ya maendeleo si tu kwa mchezaji bali kwa klabu nzima kwa ujumla,".
  "Hajib anashinda tunzo hii kwa mara ya pili mfululizo. Wote mtakubaliana nami kuwa kwa kiwango anachoonesha mshambuliaji Ajib ni kweli mshabiki, wanachama na wapenzi wa Simba hawajakosea kumchagua tena mshambuliaji wetu huyu,”
  Aveva pia ametoa wito kwa wachezaji wengine wote wa Simba kuendelea kujituma zaidi, kwa kuwa uongozi na mashabiki wana matumaini makubwa msimu huu, wakiamini juu ya kaulimbiu yao; SIMBA NGUVU MOJA.
  Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EAG Group ambao ni washauri na watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba, Imani Kajula amesema; “EAG Group inapenda kusisitiza kuendelea kuongeza utayari wake katika kushirikiana na klabu ya Simba kwenye kutoa motisha kwa wachezaji wa Simba ambapo italeta chachu ya kufanya vizuri zaidi na hivyo kuweza kutengeneza mfumo mzuri wa kuongeza vyanzo vya mapato na hatimaye faidi kubwa kwa wachezaji na timu kwa ujumla” amesema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAJIB AWEKA 'BONGE LA REKODI' SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top