• HABARI MPYA

    Sunday, March 20, 2016

    AZAM FC YASONGA MBELE AFRIKA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    AZAM FC imefanikiwa kuingia Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-3.
    Azam FC leo imeifunga Bidvest 4-3 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano ikitoka kushinda 3-0 katika mchezo wa kwanza, ugenini mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
    Sasa timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na family yake itakutana na Esperance ya Tunisia katika Raundi ya Pili mwezi ujao.
    Azam FC ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao, mfungaji mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 22 akimalizia kwa kichwa krosi ya kiungo Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Kipre Tchetche (kushoto) akipongezwa na wachezaji wenzake, Ramadhani Singano 'Messi' na Allan Wanga (kulia) baada ya kukamilisha hat trick yake


    Kipre Tchetche akamtoka beki wa kulia wa Bidvest na kuingia ndani kumpasia Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao pili dakika ya 42.
    Mcheaji wa kikosi cha kwanza cha Bidvest, Jabulani Shongwe aliyeingia dakika ya 43 kuchukua nafasi ya Pule Maliele, akaifungia timu yake sekunde chache baadaye dakika hiyo kwa shuti kali akiwa amezungukwa na mabeki wa Azam.
    Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Azam FC watulie kidogo na kuanza kucheza kwa uwiano mzuri wa kushambulia na kujilinda.
    Kipindi cha pili, Azam FC wakaendelea kung’ara baada ya Kipre Tchetche kufunga bao la tatu dakika ya 56, akimlamba chenga kipa wa Bidvest, Barr Jethren na kufunga akiwa amebaki na nyavu, kufuatia pasi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’. 
    Hata hivyo, Bidvest wakatumia makosa ya safu ya ulinzi kupooza kupata bao la pili lililofungwa na Mosiatlhaga Koiekantse dakika ya 58, akimalizia pasi ya Botes Henrico.
    Kipre Tchetche akakamilisha hat trick yake dakika ya 88 kwa kufunga bao zuri la tatu, baada ya pasi ya Sure Boy na kumchambua kipa Barr Jethren.
    Botes Henrico akaruka juu peke yake kuifungia Bidvest bao la tatu dakika ya 90, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Lecki Markus. 
    Bidvest ilitumia wachezaji wengi wa kikosi cha wachezaji wa akiba katika mechi zote mbili, ingawa leo kidogo walionekana wachezaji kama watano wa kikosi cha kwanza – na hiyo ni kwa sababu hawana malengo na michuano hiyo. 
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Serge Wawa, Kipre Bolou/Farid Mussa dk75, Ramadhani Singano ‘Messi’, Himid Mao/Jean Baptiste Mugiraneza dk59, John Bocco/Allan Wanga dk 78, Kipre Tchetche na Salum Abubakar ‘Sure Boy’. 
    Bidvest Wits: Barr Jethren, Lecki Markus, Gome Wangu, Pule Maliele/Jabulani Shongwe dk43, Jordan Liam, Nhlapo Siyabonga, Ntsundwana Somila/Botes Henrico dk46, Mosiatlhaga Koiekantse, Bhasera Onismor, Khumalo Bongani na Sekese Paseka/Mkatshana Luvuyo dk58.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YASONGA MBELE AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top