• HABARI MPYA

    Monday, October 05, 2015

    KWA WASANII HAKUNA URAFIKI, WALA UADUI WA KUDUMU

    UKISHANGAA ya Ally Chocky kufanya kazi tena na Asha Baraka baada ya viapo vya kutozikana, basi utastajabu ya Wema Sepetu kuwa adui na Kajala licha ya kulipiana faini za mamilioni ya shilingi kwenye kesi iliyokuwa mbioni kumpeleka mtu jela.
    Kuna wasanii wengi sana wanapita kwenye safari ya urafiki mkubwa huku wengine wakiishi kwenye uadui uliopindukia baina yao lakini kamwe huwa hakuna mwamana wa hali hiyo kudumu milele.
    Na ndio maana mara kadhaa tumeshuhudia karata zikigeuka, waliokuwa maadui wanakuwa marafiki na waliokuwa marafiki wanakuwa maadui – wasanii hawatabiriki, hawana tofauti na wanasiasa.

    Wakati Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa akijiunga na upinzani, viongozi wa vya upinzani walinukuliwa wakisema “Kwenye siasa hakuna urafiki wala uadui wa kudumu” wakitumia kauli hiyo kufafanua ni kwanini wamekubali kufanya kazi na Lowassa wakati alikuwa mmoja wa wanasiasa waliokuwa wakimpiga ‘nondo’ za kufa mtu.
    Mwanasiasa kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili ni jambo la kawaida na huwa halijalishi vita vyao vya hapo kabla.
    Na hivyo ndivyo ninavyowafananisha wasanii na wanasiasa, ukiingilia vita vya wasanii basi unatakiwa utumie akili ya ziada vinginevyo mwisho wa siku utaonekana punguani.
    Kuingilia ugomvi wa wasanii ni sawa na kuingilia ugomvi wa wana ndugu – Si unakumbuka bifu la Mzee Yussuf na dakake Hadija Yussuf wakati Five Stars Modern Taarab inaanzishwa, wako wengi waliofurahia ugomvi ule wakiamini utadumu milele na milele lakini mwisho wa siku wanandugu hao wakapatana  na kuibuka na wimbo “Wagombanao” mahasidi wote wakabaki midomo wazi.
    Leo hii ukijaribu kumvuruga Isha Mashauzi na mdogo wake Saida Ramadhan basi ujue mwisho wa siku utaumbuka, hakuna jambo linashinda nguvu ya undugu.
    Wako mashabiki uchwara wa muziki na sanaa kwa ujumla wake ambao kutokana na kukosa kwao kazi za kufanya, basi hulazimisha kukuza majina yao kwa kushabikia bifu za wasanii.
    Mbaya zaidi mashabiki hawa si aina ya mashabiki wanaonunua kazi za msanii au kuchangia kipato cha msanii kwa aina yoyote, si wa kwenda ukumbini wala si wa kuingia dukani na kununua kazi ya msanii.
    Wengi wao ni mashabiki wasiowajua wasanii zaidi ya kuwasikia redioni, kuwaona kwenye televisheni na kuwasoma magazetini, lakini wao ndio watakaojivisha mabomu na kukomalia vita vya wasanii kuliko hata wasanii wenyewe.
    Watu hawa ni aina ya mashabiki wanaorudisha nyuma sanaa ya Tanzania badala ya kuipeleka mbele, ni watu wanaotafuta umaarufu kinyemela kwa kutumia mwamvuli wa ushabiki.
    Sanaa yetu inadidimia siku hadi siku, inamezwa na utamaduni wa nje na hivyo huu ni wakati muafaka wa kuibuka na hoja zenye mashiko kwa wasanii wetu, kuwapa moyo na kuwaelimisha kwa njia zinazojenga badala ya kusubiri bifu za wasanii na kuzifanya ndio habari ya mjini.
    Niliwahi kusema hapo nyuma kuwa wako wasanii wanaokonda kwa mafanikio ya wasanii wenzao, lakini leo namba niongezee nyama kidogo – wako pia mashabiki wanaopata vidonda vya tumbo kwa mafanikio ya wasanii wasiowashabikia.
    Ugomvi wa wasanii uchukulie kwa mfano ule ule wa ndugu wagombanapo – tunaambiwa chukua jembe ukalime, wakipatana chukua kapu ukavune. Hizo ndio salam zangu kwa mashabiki uchwara, tukutane Jumatatu ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA WASANII HAKUNA URAFIKI, WALA UADUI WA KUDUMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top