• HABARI MPYA

    Monday, March 11, 2019

    YANGA SC WATOZWA FAINI SH MILIONI 6 KWA KUINGILIA MLANGO USIO RASMI MECHI NA SIMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Yanga imetozwa faini ya jumla ya Sh. Milioni 6 kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi kwenye mechi namba 270 wakichapwa 1-0 na mahasimu wao wa jadi, Simba SC. 
    Pamoja na kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani, Yanga pia wametiwa hatiani kwa kutoingia vyumbani na kusababisha wachezaji wakaguliwe kwenye korido, na pia kutotumia njia maalum iliyowekwa kwa ajili ya kuingia kwenye eneo la kuchezea katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 16, 2019 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Machi 7, 2019 ilipitia matukio mbalimbali ya Ligi pamoja na malalamiko yaliyowasilishwa mbele yake.

    Katika kikao hicho, Simba nayo imetozwa faini ya Sh. Milioni 3 kwa kuingia uwanjani wakitumia mlango usio rasmi, lakini vilevile kutotumia njia maalum iliyowekwa kwa ajili ya kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch). 
    Adhabu kwa timu zote zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 244- Kagera Sugar 0 vs Mbeya City 1; Kocha wa Mbeya City, Ramadhan Nsanzurwimo amepewa Onyo Kali kwa kutoa maelekezo kwa timu yake wakati akiwa jukwaani akitumikia adhabu ya kufungiwa katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 6, 2019 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. 
    Adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Mechi namba 245- Azam FC 1 vs Alliance FC 1. Kocha Malale Hamsini wa Alliance FC amefungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kwenda kwenye uzio unaotenganisha wachezaji na washabiki, na kuanza kuzozana na washabiki wa Azam FC katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 6, 2019. 
    Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Mechi namba 251- JKT Tanzania 0 vs Yanga 1. Klabu ya Yanga imetozwa faini ya sh. 1,500,000 (milioni moja na nusu) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa ukaguzi na wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 10, 2019 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 
    Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 265- Mbeya City 1 vs Stand United 1. Mchezaji Yusuph Abdallah wa Mbeya City amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Stand United katika mchezo huo uliofanyika Februari 15, 2019 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya. 
    Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
    Mechi namba 272- Mwadui FC 2 vs Biashara United 1. Klabu ya Biashara United imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuvamia chumba cha timu ya Mwadui FC kutokana na imani za kishirikina katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 19, 2019 kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
    Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu. Mechi namba 274- Mbao FC 1 vs Yanga 2. Klabu ya Yanga imetozwa faini ya sh.  500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuvamia eneo la kuchezea (pitch)  kushangilia ushindi mara baada ya kumalizika mechi hiyo iliyofanyika Februari 20,  2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 
    Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu. Mechi namba 275- Ndanda 2 vs Singida United 0. Kocha Dragan Popadic wa Singida United FC amefungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kupinga maamuzi ya Mwamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 20, 2019 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. 
    Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha. Mechi namba 277- Coastal Union 1 vs Azam FC 1. Kocha wa Azam FC, Hans van Pluijm na wachezaji wake Ramadhan Singano, na Stephen Kingue wamepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kuwavamia na kuwazonga waamuzi katika eneo la kuchezea (pitch) baada ya filimbi ya mwisho katika mchezo huo uliofanyika Februari 19, 2019 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Mechi namba 162- Azam FC 1 vs Simba 3. Klabu ya Azam imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, na kutoingia vyumbani hivyo kusababisha wachezaji wakaguliwe kwenye korido katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 22, 2019 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mechi namba 283- Ruvu Shooting 6 vs Mwadui FC 2. Kocha Ally Bizimungu wa Mwadui FC amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuwazonga waamuzi vyumbani mwao kabla ya kuanza kipindi cha pili, na pia kumfokea Mwamuzi Msaidizi, hivyo Mwamuzi kumtoa kwenye benchi katika mechi hiyo iliyofanyika Machi 2, 2019 kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani. 
    Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha. Mechi namba 288- Kagera Sugar 2 vs Lipuli 0. Kocha Msaidizi wa Lipuli FC, Selemani Matola amefungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kupinga maamuzi ya Mwamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Machi 3, 2019 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. 
    Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha Ligi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WATOZWA FAINI SH MILIONI 6 KWA KUINGILIA MLANGO USIO RASMI MECHI NA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top