• HABARI MPYA

    Wednesday, March 20, 2019

    HASSAN KESSY NA NKANA FC YAKE KUMENYANA NA CS SFAXIEN YA TUNISIA KOMBE LA SHIRIKISHO

    Na Mwandishi Wetu, CAIRO
    BEKI Mtanzania, Hassan Ramadhani Kessy, timu ya Nkana FC ya Zambia itamenyana na CS Sfaxien ya Tunisia katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwezi ujao.
    Katika droo iliyopangwa leo ukumbi wa Aida Ballroom, Marriot Zamalek mjini Cairo, Misri, Nkana FC itaanzia nyumbani mjini Kitwe Aprili 7 kabla ya kwenda Tunis Aprili 14 kwa mchezo wa marudiano.
    Mechi za Robo Fainali Kombe la Shirikisho, Etoile du Sahel ya Tunisia itamenyana na Al-Hilal ya Sudan, Hassania Agadir na Zamalek ya Misri, Gor Mahia ya Kenya na RS Berkane ya Morocco.
    Ikienda Nusu Fainali Nkana FC itamenyana na mshindi kati ya Gor Mahia na RS Berkane, wakati mshindi kati ya Etoile du Sahel na Al-Hilal atamenyana na mshindi kati ya Hassania Agadir na Zamalek, mechi za kwanza zikichezwa Aprili 28 na marudiano Mei 5.

    Hassan Kessy ataiongoza Nkana FC dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho  

    Fainali ya kwanza ya Kombe la Kombe la Shirikisho msimu wa 2018-2019 itachezwa Mei 19 na marudiano yatakuwa Mei 26.
    Nkana imefika hatua hii baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi C kwa pointi zake tisa, nyuma ya Al-Hilal iliyomaliza kileleni kwa kwa pointi zake 11 na mbele ya Asante Kotoko ya Ghana iliyomaliza na pointi saba sawa na timu nyingine ya Zambia, ZESCO United.
    Na hiyo ni baada ya kuitoa FC San Pedro ya Ivory Coast katika mchujo wa kuwania hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kwa mabao 3-0 iliyoshinda Kitwe kabla ya kwenda kutoa sare ya 0-0 mjini San-Pedro.
    Na hiyo ilifuatia kutolewa na Simba SC ya Tanzania katika hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya 4-3, wakishinda 2-1 Kitwe na kufungwa 3-1 Dar es Salaam, wakitoka kuitoa UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1, wakishinda 2-1 ugenini na 1-0 nyumbani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HASSAN KESSY NA NKANA FC YAKE KUMENYANA NA CS SFAXIEN YA TUNISIA KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top