• HABARI MPYA

    Saturday, March 30, 2019

    WANACHOTAKIWA KUFANYA YANGA KATIKA WAKATI HUU MGUMU KWAO

    Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
    KWA siku za karibuni timu ya Yanga SC imekuwa ikikabiliwa na timbwili kuanzia kwa uongozi, benchi la ufundi na hata wachezaji, hali inayowaumiza sana mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini.
    Ukiachana na ukata unaoikabili klabu hiyo kwa sasa, suala la viongozi kujiengua limezidi kuzua taharuki kwa wapenzi wa timu hiyo. Kujiuzulu kwa Samwel Lukumayi aliyekuwa makamu Mwenyekiti na Hussein Nyika aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya mashindano, usajili na mjumbe wa kamati ya utendaji, kumeibua maswali mengi.
    Huku hayo yakiendelea, tetesi za baadhi ya wachezaji wa Yanga kuhusishwa kutaka kujiunga na Simba SC, zimezidi kuwapasua zaidi vichwa wanajangwani hao. 
    Ibrahim Ajibu anatakiwa na klabu yake ya zamani, Simba SC na Gardiel Michael amekwenda Afrika Kusini kwa majaribio

    Kumekuwa na tetesi kwamba kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib, beki Kelvin Yondani na kiungo mkongomani Pappy Kabamba Tshishimbi wanahitajika mtaa wa pili. 
    Hayo yote ukiongeza na shinikizo kutoka kwa kocha Mwinyi Zahera juu ya malipo ya mishahara ya wachezaji, yamezidi kuleta sintofahamu wakati huu ambapo ligi inakaribia kufika kileleni.
    Wanachopaswa kufanya Yanga sasa hivi ni kutulia kujikita zaidi katika ligi na michuano ya ya shirikisho (ASFC). 
    Ni kweli Yanga iko katika wakati mgumu kifedha. Sikatai kwamba Yanga inahitaji uongozi utakaoleta mapinduzi ya namna ya kuendesha klabu hiyo. Lakini wakati wanasubiri Aprili 28 ifike ili wafanye uchaguzi, lazima wafanye jambo la busara, hekima na utulivu ili kudumisha umoja miongoni mwao.
    Jumamosi hii kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wananchi hao watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Alliance FC katika robo fainali ya ASFC. Hii ni mechi muhimu sana kwa Yanga ukizingatia kwamba msimu huu wameshindwa kushiriki michuano ya kimataifa. Hivyo wanafanya kila namna ili hata kama wakikosa ubingwa wa TPL, basi kombe la shirikisho walibebe ili mwakani waiwakilishe nchi.
    Jambo jingine linalotia moyo ni kwamba Yanga bado inaongoza ligi, hivyo lolote linaweza likatokea. Cha msingi watulie na kuweka nguvu nyingi zaidi kwenye michuano hii halafu mambo mengine baadaye.
    Nitoe tu wito kwa viongozi, wachezaji na wapenzi wa Yanga kuwa na utulivu ili washinde mechi zao halafu suala la kumtafuta mchawi litajulikana baadaye. Kama ambavyo motto wao unavyosema "Daima mbele, nyuma mwiko" na iwe hivyo kwelikweli. 
    Vichwa vya habari kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari visiwachanganye kwa sasa. Mnapaswa kujua mnatafuta nini na mnapaswa kufanya nini kwa wakati huu. Msiangalie kwamba wapinzani wenu wamefanya nini. Hayo hayawahusu kwa sasa. Mafanikio yao ni ya kwao tu, yasiwafanye mkakonda bure. Yanga inapaswa kupiga hatua kusonga mbele kwani kwao nyuma ni mwiko na marufuku.
    (Mwandishi wa makala hii, Frederick Daudi anapatikana kwa namba +255 742 164 329 na barua pepe defederico131@gmail.com)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANACHOTAKIWA KUFANYA YANGA KATIKA WAKATI HUU MGUMU KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top