• HABARI MPYA

    Thursday, March 14, 2019

    WAZIRI MAKAMBA NDIYE MGENI RASMI MECHI YA SIMBA SC DHIDI YA AS VITA JUMAMOSI TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano, January Yussuf Makamba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Taarifa ya Simba SC leo imesema kwamba, Makamba ambaye ni mpenzi na mwanachama wa klabu hiyo atakaa pamoja na watazamaji watakaolipa tiketi za Platnums Jumamosi zinazouzwa Sh. 100,000 
    Kiingilio cha chini katika mchezo huo kitakuwa ni Sh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko, wakati VIP A Sh. 20,000 na VIP B, Sh. 10,000.
    Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano, January Makamba atakuwa mgeni rasmi Simba na Vita Jumamosi Uwanja wa Taifa 

    Mchezo huo utakaoanza Saa 1:00 usiku, utachezeshwa na marefa wa Morocco, Noureddine El Jaafari atakayepuliza kipyenga na washika vibendera Hicham Ait Abbou na Yahya Nouali.
    Simba SC inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kutinga Robo Fainali, baada ya kupoteza mechi zake zote tatu za ugenini, 5-0 mara mbili dhidi ya Al Ahly nchini Misri na AS Vita mjini Kinshasa na 2-0 dhidi ya JS Saoura mjini Bechar. 
    Kwa sasa JS Saoura ndiyo inayoongoza Kundi D kwa pointi  zake nane baada ya kucheza mechi tano, ikifuatiwa na Al Ahly, AS Vita zenye pointi saba kila moja, wakati Simba SC inashika mkia katika kwa pointi zake sita.
    Wakati Simba SC ikimaliza na AS Vita mjini Dar es Salaam, Al Ahly watakuwa wenyeji wa JS Saoura Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria nchini Misri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZIRI MAKAMBA NDIYE MGENI RASMI MECHI YA SIMBA SC DHIDI YA AS VITA JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top