• HABARI MPYA

    Wednesday, March 20, 2019

    TAMASHA LA UTAMADUNI LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUFANYIKA SEPTEMBA 21 HADI 28 DAR

    Na Shamimu Nyaki-WHUSM
    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalojulikana kama JAMAFEST linatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 21-28 mwaka huu.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Dkt.Mwakyembe ameeleza kuwa Tamasha hilo linaloongozwa na Kauli mbiu “Uanuai wa Kitamaduni;Msingi  wa Utengamano wa Kikanda,Maendeleo ya Kiuchumi na Kushamiri kwa Utalii. Lengo lake ni kulinda na kuendeleza Urithi wa Utamaduni na kukuza utambulisho wa Afrika Mashariki.
    Ameendelea kueleza kuwa Tamasha hilo litawezesha uhamasishaji wa Sanaa na Utamaduni kwa kutangaza vivutio vya kitalii na utamaduni vilivyopo nchini,kutangaza fursa za kiuchumi na kijamii pamoja na mandhari mazuri ya upigaji picha na filamu kwa wadau wa kitaifa kikanda na kimataifa.
    Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema Tamasha la JAMAFEST litafanyika kuanzia Septemba 21 hadi 28 mwaka huu

    “Tamasha litaunganishwa na matamasha mengine ya  Utamaduni nchini ikwemo Usiku wa tuzo za Serengeti International Film Festival pamoja na tukio la watu sita watakaopanda Mlima Kilimanjaro na kupeperusha bendera za nchi zao juu ya kilele cha Mlima huo kuashiria uzinduzi wa Tamasha hilo la JAMAFEST”alisema Dkt.Mwakyembe.
    Mhe. Mwakyembe ameendelea kueleza kuwa Tamasha hilo litakuwa na maonesho mbalimbali ya kiutamaduni ikiwemo mavazi asili, sanaa ya uchongaji,wabunifu wa vifaa vya mapambo,michezo ya kuigiza watunga riwaya na mabingwa wa lugha ya Kiswahili,watengenezaji wa vyakula na michezo mbalimbali ya Jadi.
    Aidha Dkt. Mwakyembe ameisitiza Watanzania kushiriki katika tamasha hilo kwa  kuuza na kutangaza kazi zao za Sanaa na Utamaduni kwani nchi yetu mwaka huu imebahatika kuwa na matukio makubwa yenye fursa ya kuitangaza nchi ikiwemo Sekta ya Michezo kwani timu ya Taifa Stars na Serengeti Boys zinatarajiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya Afrika ya AFCON.
    Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Bibi.Joyce Fissoo amesema kuwa Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini ambapo nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki za Kenya,Uganda,Rwanda,Burundi Sudan Kusini na Mwenyeji Tanzania zinatarajiwa kushiriki.
    Bibi Fissoo ameendelea kueleza kuwa Tamasha hilo lilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Rwanda mwaka 2013 ambalo lilihudhuriwa na washiriki17,500 Kenya ikafuatia mwaka 2015 kwa kuwa na washiriki 21,000 na Uganda mwaka 2017 ambapo washiriki 42,600 walijitokeza.
    “Tamasha hili linafanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi hizo wanachama wa Jumiya ya Afrika Mashariki kwa kila baada ya miaka miwili kwa mujibu wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki la mwaka 2012”.aliongeza Bi Fissoo.
    Tamasha hilo linaratibiwa na Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara nyingine,pamoja na Kamati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi wanachama.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAMASHA LA UTAMADUNI LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUFANYIKA SEPTEMBA 21 HADI 28 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top