• HABARI MPYA

    Thursday, March 14, 2019

    UWANJA MPYA WA MICHEZO DODOMA KUWA NA MWONEKANO WA MLIMA KILIMAJARO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UWANJA mpya wa michezo nchini utakaojengwa mjini Dodoma utakuwa na mwonekano wa Mlima Kilimanjaro.
    Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale mjini Dar es Salaam jana katika kikao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli.
    Mhandisi Patrick Mfugale alisema kwamba Uwanja huo utajengwa jirani na eneo la Nanenane kando ya barabara ya Dodoma – Morogoro, utajengwa kwa mfano wa mlima Kilimanjaro na utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji kati ya 85,000 na 100,005.

    Rais Dk. Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu wa Tanzania na Morocco wanaoshughulikia ujenzi wa Uwanja huo unaotarajiwa kujengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI.
    Balozi wa Morocco hapa nchini aliyeongoza ujumbe wa wataalamu kutoka Morocco, Abdelilah Benryane alisema pamoja na kuzungumzia uhusiano mzuri wa Tanzania na Morocco wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa wakati wa ziara ya Mfalme wa Morocco hapa nchini mwaka 2016 ikiwemo ujenzi wa Msikiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa Jijini Dar es Salaam na kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Jijini Dodoma.
    Katika kikao chake na Rais Dk. Magufuli Ikulu mjini Dar es Salaam Oktoba 25 mwaka 2016, Mfalme Mohammed V aliahidi kuijengea Tanzania Uwanja wa michezo kwa gharama ya dola za Kimarekani Milioni 100.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UWANJA MPYA WA MICHEZO DODOMA KUWA NA MWONEKANO WA MLIMA KILIMAJARO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top