• HABARI MPYA

    Monday, March 25, 2019

    RAIS MAGUFULI AWAZAWADIA VIWANJA DODOMA WACHEZAJI TAIFA STARS KWA KUFUZU AFCON

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli ameagiza wachezaji wote wa timu ya taifa, Taifa Stars iliyofanikiwa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Juni mwaka nchini Misri wapatiwe viwanja katika eneo zuri mjini Dodoma.
    Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu mjini Dar es Salaam leo alipokutana na wachezaji wa Taifa Stars kuwapongeza kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda usiku wa jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam hivyo kuiwezesha nchi kufuzu AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya kiungo wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Happygod Msuva na mabeki, Erasto Edward Nyoni wa Simba SC na Aggrey Morris Ambroce wa Azam FC za nyumbani, Tanzania na Uganda kufuzu kutoka Kundi L.

    Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli akiwa na wachezaji wa Taifa Stars Ikulu mjini Dar es Salaam leo

    Taifa Stars imefuzu kama mshindi wa pili wa kundi kwa pointi zake nane, nyuma ya Uganda iliyomaliza na pointi 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
    Pamoja na wachezaji, ofa ya viwanja wamepewa pia wachezaji wawili waliokuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars iliyofuzu AFCON ya mwaka 1980, beki Leodegar Tenga na mshambuliaji, Augustino Peter, maarufu kama Peter Tino.
    Ofa ya kiwanja amepewa pia bondia Hassan Mwakinyo aliyealikwa pia Ikulu leo baada ya kumshinda kwa Knockout (KO) raundi ya tano Muargentina, Sergio Eduardo Gonzalez juzi mjini Nairobi nchini Kenya.
    Kwa Peter Tino, pamoja na kiwanja Rais Magufuli alimzawadia fedha taslimu Sh. Milioni 5 kama mtaji wa kwenda kufanya biashara ya kuendesha maisha yake. 
    Kwa wachezaji, mbali ya zawadi ya viwanja ya Rais, kila mmoja atapatiwa donge nono la Sh. Milioni 10, ahadi ya Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, chini ya Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.  
    Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa ameshauri ya Saidia Taifa Stars Ishinde, chini ya Mwenyekiti wake, Makonda iendelee na jukumu hilo na kwamba ihusishwe pia kwenye kampeni za timu nyingine za taifa na hata klabu ikibidi.  
    Kwa ujumla mbio za kuwania tiketi ya AFCON 2019 zilikamilishwa jana huku timu nne za Afrika Mashariki, Burundi Uganda, Kenya na Tanzania zikifuz fainali za mwaka huu zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19.
    Kutoka kundi A zilizofuzu ni Senegal na Madagascar zilizozipiku Equatorial Guinea na Sudan, kutoka Kundi B Morocco na Cameroon zilizozipiku Malawi na Comoro, kutoka Kundi C Mali na Burundi zilizozipiku Gabon na Sudan Kusini, kutoka Kundi D Algeria na Benin zilizozipiku Gambia na Togo na Kundi E ni Nigeria na Afrika Kusini zilizozipiku Libya na Shelisheli.
    Nyingine ni kutoka Kundi F ambazo ni Ghana na Kenya zilizozipiku Ethiopia na Sierra Leone, kutoka Kundi G Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zilizozipiku Liberia na Kongo, kutoka Kundi H ni Guinea na Ivory Coast zilizozipiku Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Rwanda.
    Nyingine ni kutoka kutoka Kundi I Angola na Mauritania zilizozipiku Burkina Faso na Botswana, kutoka Kundi J Tunisia na Misri zilizozipiku Niger na Eswatini, kutoka Kundi K Guinea-Bissau na Namibia zilizozipiku Msumbiji na Zambia na kutoka Kundi L Uganda na Tanzania zilizopiku Lesotho na Cape Verde.
    Droo ya kupanga makundi ya AFCON ya mwaka huu ambayo kwa mara ya kwanza itashirikisha timu 24 kutoka 16, itafanyika 12 Aprili 12 mjini Cairo nchini Misri.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AWAZAWADIA VIWANJA DODOMA WACHEZAJI TAIFA STARS KWA KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top