• HABARI MPYA

  Monday, March 11, 2019

  MCHEZAJI WA PAMBA SC APELEKWA KAMATI YA NIDHAMU KWA KUTAKA KUWAPIGA WAAMUZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZAJI Deus Tulusubya wa Pamba SC ya Mwanza amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kutaka kuwapiga waamuzi katima mechi namba 88 ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara timu yake ikichapwa 2-1 na Mashujaa FC ya Kigoma Machi 2, 2019 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
  Taarifa ya Afisa Habari Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo kwa Vyombo vya Habari leo imesema kwamba mechi namba 80- Klabu ya Mlale FC imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) ikitoa sare ya 1-1 na Mlale FC baada ya washabiki wake kuwavamia wale Mawenzi SC na kuanza kuwapiga katika mchezo uliofanyika Februari 16, Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. 

  Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Klabu. Naye Kamishna wa mechi hiyo, Bw. Nassoro Kipenzi kutoka Dodoma ameondolewa kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu kuhusu tukio hilo.
  Mechi namba 84- Mbeya Kwanza 1 vs Reha FC 0;  Mchezaji Idrissa Ramadhan Ally wa Reha FC amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kumpiga kichwa mchezaji mmoja wa Mbeya Kwanza katika mechi hiyo iliyofanyika Februari 16, 2019 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
  Nayo klabu ya Mbeya Kwanza imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya washabiki wake kuvamia uwanja (pitch) kushangilia bao la timu hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
  Mechi namba 73- Pamba SC 1 vs Transit Camp 0; Klabu ya Transit Camp imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na viongozi wa benchi la ufundi kumzonga Mwamuzi baada ya mchezo huo uliofanyika Februari 9, 2019 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
  Mechi namba 74- Polisi Tanzania 1 vs Geita Gold 0; Klabu ya Polisi Tanzania imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kufanya vitendo vilivyoashiria imani za kishirikina ikiwemo kuvunja mayai kwenye kona ya uwanja katika mchezo huo uliofanyika Februari 9, 2019 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
  Mechi namba 76- Rhino Rangers 0 vs Dodoma FC 0; Klabu ya Dodoma FC imepewa Onyo baada ya kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 16 katika mchezo huo uliofanyika Februari 9, 2019 Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
  Mechi namba 80- Arusha United 1 vs Green Warriors 0. Klabu ya Green Warriors imetozwa faini ya sh. 1,500,000 (milioni moja na nusu) kwa timu yake kugoma kuingia vyumbani, hivyo kusababisha ikaguliwe ikiwa nje katika mchezo huo uliofanyika Februari 16, 2019 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.  Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
  Mechi namba 82- Mgambo Shooting 0 vs Pamba SC 1; Mchezaji Rashid Ally wa Mgambo Shooting amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji Elias Seth wa Pamba SC baada ya kumalizika mchezo huo uliofanyika Februari 16, 2019 Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MCHEZAJI WA PAMBA SC APELEKWA KAMATI YA NIDHAMU KWA KUTAKA KUWAPIGA WAAMUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top