• HABARI MPYA

  Saturday, April 07, 2018

  YANGA SC YABISHA HODI HATUA YA MAKUNDI AFRIKA…YAWAPIGA WAHABESHI 2-0 TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wolaita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua hiyo jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo uliotokana na mabao ya Raphael Daudi kipindi cha kwanza na Emmanuel Martin kipindi cha pili, unamaanisha Yanga SC watahitaji kwenda kulazimisha sare ugenini wiki ijayo, au kutofungwa zaidi ya tofauti ya bao moja ili kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili baada ya mwaka 2016.
  Daudi aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC baada ya kusajiliwa kutoka Mbeya City leo alichezeshwa katika nafasi ya ushambuliaji badala ya sehemu yake ya kiungo na akafunga dakika ya kwanza tu akimalizia krosi ya beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali. 
  Wafungaji wa mabao ya Yanga leo, Emmanuel Martin (kulia) na Raphael Daudi (kushoto) wakipongezana baada ya bao la pili 
  Nyota wa mchezo wa leo, Yussuf Mhilu wa Yanga akimtoka beki wa Wolaita Ditcha, Tesfu Elias
  Raphael Daudi (kulia) baada ya kumpiga chenga beki wa Wolaita Ditcha, Haymanot Worko
  Kiungo wa Yanga, Ibrahim Ajib akiwatoka wachezaji wa Wolaita Ditcha
  Kiungo wa Yanga, Pius Buswita akijaribu kumpiga chenga beki wa Wolaita Ditcha, Abdulsemed Ali

  Bao hilo la mapema liliwajengea hali ya kujiamini wachezaji wa Yanga na kupeleka mashambulizi zaidi mfululizo langoni mwa Wolaita Dictha, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi.
  Lakini baadaye Wolaita wakatulia na kuanza kucheza mpira wao mzuri wa kupasiana kuanzia kwenye eneo lao hadi la wapinzani na kulitia misukosuko lango la Yanga.
  Sifa zimuendee kipa Mcameroon, Youthe Rostand Jehu aliyefanya kazi nzuri leo pamoja na mabeki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
  Kipindi cha pili, Yanga walikianza vizuri tena na kufanikiwa kupata bao la mapema, safari hiyo winga Emmanuel Joseph Martin kumalizia kwa kichwa krosi ya kiungo wa pembeni, Yussuf Mhilu kufunga bao la pili dakika ya 54.  
  Lilikuwa bao ambalo lilizidi kuwajengea hali ya kujiamini Yanga na kuwakatisha tamaa Ditcha, hivyo mabingwa hao wa Tanzania kuzidi kuutawala mchezo, lakini wakashindwa tu kuongeza bao.
  Pamoja na hayo, Wolaita Ditcha ikiongozwa na mshambuliaji wake, Mtogo Arafat Djako ilikaribia kufunga mara mbili, kama si juhudi za kipa Rostande kuokoa michomo miwili ya hatari.
  Yanga ilipata pigo dakika ya 74, baada ya beki wake, Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Nahodha na mkongwe, Nadri Haroub ‘Cannavaro’ aliyekwenda kumalizia vizuri akicheza na Mzanzibar mwenzake, Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
  Timu hizo zitarudiana na Jumatano ijayo, Aprili 18 Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa, Ethiopia na mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na kuzawadiwa kitita cha sola za Kimarekani 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Andrew Vincent ‘Dante’/Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dk74, Thabani Kamusoko/Pato Ngonyani dk76, Yussuf Mhilu, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk88, Pius Buswita, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin. 
  Wolaita Ditcha; Wond Wosen Geremen, Mubarik Shikori, Haymanot Worko, Wubishet Alemayenu, Bezabih Malayu, Temesgen Duba/Eyob Alimayenu dk55, Amrala Diltata, Arafat Djako/Chernet Gugsa dk90, Yared Dawit, Abdulsemed Ali na Tesfu Elias.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YABISHA HODI HATUA YA MAKUNDI AFRIKA…YAWAPIGA WAHABESHI 2-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top