• HABARI MPYA

  Wednesday, April 04, 2018

  CAF YAWAZUIA YONDAN, TSHISHIMBI, CHIRWA NA MAKAPU KUCHEZA DHIDI YA WAHABESHI JUMAMOSI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeitumia barua ya tahadhari Yanga kutowatumia wachezaji wake wanne, mabeki Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Mzambia Obey Chirwa katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Welaita Ditcha ya Ethiopia.  
  Yanga watakuwa wenyeji wa Waleita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na barua iliyoandikwa jana kutoka makao makuu ya shirikisho, Cairo nchini Misri imesema wanne hao pamoja na wachezaji wawili wa Welaita Ditcha, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho hawaruhusiwi kucheza mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zilizopita za timu zao.
  Kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi hatakuwepo Jumamosi dhidi ya Welaita Ditcha ya Ethiopia 

  Lakini Meneja wa Yanga, Hadidh Saleh amesema ni kweli wanafahamu Makapu, Tshishimbi na Chirwa wana kadi mbili za njano, lakini kwa Yondan kumbukumbu zao zinaonyesha ana kadi moja tu.
  “Tunajaribu kuwasiliana na CAF kupata ufafanuzi, maana sisi kumbukumbu zetu zinaonyesha ana kadi moja tu,”amesema Saleh. 
  Yanga imeweka kambi mjini Morogoro tangu juzi kujiandaa na mchezo huo na inatarajiwa kurejea mjini Dar es Salaam kesho kwa maandalizi ya ‘mwisho mwisho’.
  Yanga wataingia kwenye mchezo wa Jumamosi wakitoka kutolewa na Singida United katika Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Jumapili Uwanja wa Namfua mjini Singida.
  Na Yanga waliingia kwenye mchezo huo wakitoka kutolewa kwenye hatua ya 32 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya 2-1 waliyofungwa na Township Rollers ya Botswana Machi 6 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam kabla sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CAF YAWAZUIA YONDAN, TSHISHIMBI, CHIRWA NA MAKAPU KUCHEZA DHIDI YA WAHABESHI JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top