• HABARI MPYA

    Sunday, April 08, 2018

    AZAM YAZIDI KUJITOA MBIO ZA UBINGWA, STAND UNITED YAIDIDIMIZA NJOMBE MJI FC, NGASSA AIOKOA NDANDA KUZAMA NYUMBANI

    Na Princess Asia, MBEYA
    TIMU ya Azam FC imezidi kujiondoa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Mbeya City jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Sare hiyo inaiongezea pointi moja tu Azam FC na kufikisha pointi 45 baada ya kucheza mechi 23, ikiendelea kukamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21 na vinara, Simba SC wenye poinyi 49 za mechi 21 pia.
    Mbeya City inafikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi ya 23 leo, ikibaki nafasi ya nane na Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na na Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani leo inafikisha pia pointi 25 baada ya kucheza mechi 23 na kubaki nafasi ya tisa. Prisons inafikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 23 na kubaki nafasi ya nne. 
    Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Stand United imeshinda 3-1 dhidi ya Njombe Mji FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. Mabao ya Stand yamefungwa na Suleiman Ndikumana dakika ya kwanza, Sixtus Sabilo mawili dakika ya 84 na 90, huku la Njombe Mji FC likifungwa na Nitikely Masasi dakika ya 75.
    Stand United inafikisha pointi 25 baada ya kucheza mechi 23 na kupanda hadi nafasi ya 10 kutoka ya 12, wakati Njombe Mji FC inabaki na pointi zake 18 za mechi 23 katika nafasi ya 15 kwenye Ligi Kuu ya timu 16. 
    Mkongwe Mrisho Khalfan Ngassa ameinusuru Ndanda FC kulala mbele ya Kagera Sugar baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 33 kufuatia Abdallah Mguhi ‘Messi’ kuanza kuwafungia wageni dakika ya 27 Uwanja wa Nangwnada Sijaona mjini Mtwara, timu hizo zikitoka sare ya 1-1.
    Ndanda FC inafikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 23 ikibaki nafasi ya 11, wakati Kagera Sugar inafikisha pointi 22 baada ya kucheza mechi 23 na kubaki nafasi ya 13.
    Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Owen Chaima, John Kabanda/Rajab Isihaka dk90, Hassan Mwasapili, Ally Lundenga, Ramadhan Malima, Eliud Ambokile, Majaliwa Shaban, Haruna Shamte, Victor Hangaya/Godfrey Miller dk80, Babu Ally Seif/Danny Joram dk73 na Frank Ikobela. Azam FC: Razack Abalora, Swaleh Abdallah, Salmin Hoza, Abdallah Kheri, Aggrey Morris, Himid Mao, Frank Domayo, Salim Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Idd/Joseph Kimwaga dk84, Yahya Zayed na Joseph Mahundi/Iddi Kipagwile dk66.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAZIDI KUJITOA MBIO ZA UBINGWA, STAND UNITED YAIDIDIMIZA NJOMBE MJI FC, NGASSA AIOKOA NDANDA KUZAMA NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top