• HABARI MPYA

    Saturday, January 20, 2018

    WAZIRI MWAKYEMBE AWATEMBELEA SERENGETI BOYS KAMBINI KARUME

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe leo amewatembelea wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys waliopo kambini kwenye hostel za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zilizopo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
    Katika ziara yake hiyo, Waziri Mwakyembe alijionea namna wachezaji hao wanaoshi na kufanya mazoezi chini ya walimu wao, Mdenmark Kim Poulsen na Msaidizi wake, Oscar Milambo.
    Pamoja na kuzungumza nao na kuwatia moyo ili wajitume zaidi, Waziri Mwakyembe aliwaachia ujumbe wa Serikali wachezaji wa Serengeti Boys ambao wote hawazidi umri wa miaka 16.
    Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiwasalimia wachezaji wa Serengeti Boys leo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam

    Dk. Mwakyembe akitoa salamu za Serikali amewaambia vijana wanaounda timu hiyo kuwa serikali yao inawaamini na wanalo jukumu la kuiperusha vyema bendera ya Tanzania. 
    Amewataka kupambana kwaajili ya Tanzania na kuhakikisha wanafanya vyema kwenye kila mashindano huku akiwataka makocha wa kikosi hicho kuwapa mafunzo mazuri kwa ustawi wa Vijana hao. 
    Aidha, Dk. Mwakyembe amesema anaamini Vijana hao watakuwa bora chini ya TFF iliyopo madarakani inayoongozwa na Rais Ndugu Wallace Karia. 
    "Naamini mtaimarika na kuwa bora maana hata TFF hii sasa ina ari na morali kubwa" amesema Dk. Mwakyembe. 
    Katika ziara yake hiyo Dk. Mwakyembe alipata nafasi ya kutazama Serengeti Boys ikiifunga 4-1 Makongo Sekondari katika mchezo wa kirafiki.
    Kabla ya mchezo huo Serengeti Boys walicheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Kituo cha Bombom na kutoa sare ya kufungana bao 1-1.
    Wachezaji 34 wakiwemo 30 wa ndani na makipa wane, wapo kambini Serengeti Boys tangu mwanzoni mwa mwezi hadi Januari 28, 2018 kwa maandalizi ya michuano CECAFA Challenge U-17. 
    Maandalizi hayo ya Serengeti Boys yatakwenda sambamba na kucheza mechi za kirafiki kabla ya kuhairisha kambi hiyo itakayokuwa ikifanyika mara kwa mara na mpango uliopo ni kila mwezi timu hiyo kuingia kambini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZIRI MWAKYEMBE AWATEMBELEA SERENGETI BOYS KAMBINI KARUME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top