• HABARI MPYA

  Monday, January 15, 2018

  CHIRWA AFUNGIWA MECHI TATU KWA KUMPIGA MCHEZAJI WA PRISONS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Mzambia Obrey Chirwa amefungiwa mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kukiri kosa la kumpiga mchezaji wa Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Novemba 25, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Adhabu hiyo imetolewa katika kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kilichofanyika Jumapili ya Januari 14, mwaka huu 2018 mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na kufungiwa mechi tatu, Chirwa pia ametozwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa hilo kwenye mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.
  Kamati baada ya kumsikiliza Chirwa na kupitia Video za mchezo huo pamoja na taarifa ya kamishna na Muamuzi imetoa adhabu kwa mchezaji huyo kupitia Kanuni za Ligi Kuu kanuni ya 37(7b) na kanuni za nidhamu za TFF kifungu cha 48(1d) na 48(2).
  Obrey Chirwa amefungiwa mechi tatu kwa kukiri kosa la kumpiga mchezaji wa Tanzania Prisons Novemba 25, mwaka jana

  Tayari Chirwa amekosekana kwenye mchezo mmoja wa Yanga, ikifungwa 2-0 na Mbao FC mjini Mwanza na ataendelea kukosekana katika mechi mbili zijazo dhidi ya Mwadui na Ruvu Shooting Januari 21, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Adhabu hii inaweza kumuepusha Chirwa na mashabiki wa Yanga kwa sasa ambao wana hasira naye baada ya kucheza chini ya kiwango na kukosa penalti timu hiyo ikifungwa kwa penalti 5-4 na URA ya Uganda katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita visiwani Zanzibar.
  Kabla ya hapo, Chirwa alikuwa ana mgomo wa zaidi ya wiki mbili na kurejea kwao, Zambia akishinikiza alipwe fedha zake za usajili kabla ya kufikia mwafaka na uongozi na kurejea mapema wiki iliyopita.

  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHIRWA AFUNGIWA MECHI TATU KWA KUMPIGA MCHEZAJI WA PRISONS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top