• HABARI MPYA

  Sunday, December 17, 2017

  ZANZIBAR WAFA KISHUJAA MACHAKOS, KENYA MABINGWA WAPYA CHALLENGE 2017

  Na Mwandishi Wetu, MACHAKOS
  KIPA Patrick Matasi amepangua penalti tatu kuipa Kenya, Harambee Stars ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya ushindi wa penalti 3-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.
  Matasi alipangua penalti Adeyoum Ahmed, Issa Haidari ‘Dau’ na Mohammed issa ‘Banka’ huku mbili tu za viungo Feisal Salum Abdallah na Mudathir Yahya Abbas zikimpita.
  Kipa wa Zanzibar, Mohammed Abulrahman ‘Wawesha’ alipangua penalti moja tu ya Duncan Otieno, wakati za Joackins Atudo, Wesley Arasa Onguso na Samuel Onyango zilimpita.
  Mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdul Karim Twagirumukiza aliyesaidiwa na Theo Ndagamina wote wa Rwanda na Belachew Tigle wa Ethiopia, ulikuwa mkali na timu zote zilishambuliana kwa zamu kwa muda wote.
  Wachezaji wa Zanzibar wakiwa wenye huzuni  baada ya mchezo leo Uwanja wa Kenyatta, Machakos
  Lakini ni Kenya waliotangulia kupata bao kupitia kwa Ovella Ochieng aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbaki wa mita 27 dakika ya tano kufuatia kiungo Abdulaziz Makame kumuangusha Kefa Aswani.  
  Zanzibar walipotezana kidogo baada ya bao hilo na kuwaruhusu Kenya kuutawala mchezo na kusukuma mashambulizi zaidi langoni mwao.
  Hata hivyo, baada ya dakika 10 tangu wafungwe bao hilo, Zanzibar wakatulia na kuanza kucheza kwa uelewano wakigonga pasi nyingi kama ilivyo desturi yao.
  Lakini wakiwa wametulia na kuanza kusaka bao la kusawazisha, Zanzibar wakapata pigo baada ya Makame kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, akimpisha Feisal Salum dakika ya 20.
  Bahati nzuri mabadiliko hayo ya ‘bahati mbaya’ yakawa yenye manufaa, kwani Feisal alikwenda kuiongoza timu vizuri na kuifanya Zanzibar ianze kutawala mchezo.
  Kipindi cha pili, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kadiri muda ulivyokuwa ukisogea Zanzibar walizidi kupata nguvu.  
  Kenya ilipata pigo dakika ya 61 baada ya Keffa Aswani kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Masudi Juma. 
  Jitihada za Zanzibar zilizaa matunda dakika ya 87 baada ya Khamis Mussa Makame aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Seif Abdallah ‘Karihe’ kuisawazishia Heroes akimalizia kazi nzuri ya beki wa kushoto Mwinyi Hajji Mngwali aliyewatoka wachezaji wa Kenya kabla ya kutoa pasi ya bao.
  Mchezo ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza ambako Kenya walitangulia tena kwa bao la Choka Masudi Juma dakika ya 97 aliyekutana na mpira uliopigwa na kipa  Mohammed Abulrahman ‘Wawesha’ na kuwatoka mabeki Abdallah Kheri na Issa Haidari ‘Dau’ kabla ya kufunga kiulaini.
  Khamis Mussa Makame kwa mara nyingine akaisawazishia Zanzibar dakika ya 99 akinufaika na makosa ya beki Mussa Mohammed kushindwa kuokoa vizuri krosi ya Mwinyi Hajji Mngwali.
  Kikosi cha Kenya leo kilikuwa; Patrick Matasi, Mohammed Mussa, Jockins Atudo, Nicholas Sikhayi,Weslye Arasa Onguso, Patilah Omoto, Whyvonne Kinyangi, Ovella Ochieng/Kisia Ernest dk78, George Odhiambo ‘Blackberry’/Samuel Onyango dk86, Duncan Otieno na Kefa Aswani/Masudi Juma dk63.  
  Zanzibar; Mohammed Abulrahman ‘Wawesha’, Ibrahim Mohamed, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Kheri, Issa Haidari, Abdulaziz Makame/Feisal Salum dk20, Mohamed Issa ‘Banka’, Mudathir Yahya, Ibrahim Hamad ‘Hilika’, Seif Abdallah ‘Karihe’/Khamis Mussa Makamedk56 na Suleiman Kassim ‘Selembe’/Adeyoum Seif Ahmed dk116.
  Mapema katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu, Uganda iliichapa Burundi mabao 2-1 hapo hapo Uwanja wa Kenyatta, Machakos.
  Haikuwa kazi rahisi kwa The Cranes kumaliza nafasio ya tatu, kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya Nahodha wa Burundi, Pierre Kwizera kuanza kuifungia timu yake, kabla ya Saddam Juma Ibrahim kuisawazishia Uganda dakika ya 48 na Issa Dau kufunga la ushindi dakika ya 75.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZANZIBAR WAFA KISHUJAA MACHAKOS, KENYA MABINGWA WAPYA CHALLENGE 2017 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top