• HABARI MPYA

  Sunday, December 17, 2017

  YANGA WASHINDWA KUFURUKUTA KWA POLISI TZ, SARE 0-0 UHURU

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM 
  YANGA SC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Polisi Tanzania katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
  Katika mchezo huo uliohudhuriwa na watazamaji wachache, Yanga ilishindwa kabisa kutegua mitego ya Polisi ili kupata bao.
  Pamoja na benchi la ufundi la Yanga kubadili karibu wachezaji wote kipindi cha pili, akiwaningiza nyota wa kikosi cha kwanza akina Youthe Rostande, Papy Kabamba Tshishimbi, Geoffrey Mwashiuya na Burhan Akilimali kuchukua nafasi za Benno Kakolanya, Hassan Kessy, Maka Edward na Yusuph Mhilu, lakini mambo yaliendelea kuwa magumu.

  Amissi Tambwe alikaribia kufunga leo Yanga ikilazimishwa sare ya 0-0 na Polisi Uwanja wa Uhuru

  Kiungo Pius Buswita aliikosesha Yanga bao la wazi dakika ya 57 baada ya kushindwa kumalizia krosi ya Geoffrey Mwashiuya.
  Akicheza kwa mara ya kwanza msimu huu, mshambuliaji Mrundi Amissi Joselyn Tambwe aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu alikaribia kufunga dakika ya 64 kama si mpira alioupiga kwa kichwa kufuatia krosi ya Burhan Akilimali kwenda nje.
  Polisi nao walikaribia kupata bao dakika ya 66 baada ya shuti la Ahmad Kambangwa kwenda nje sentimita chache.
  Buswita tena dakika ya 76 akaunganishia nje kwa shuti dhaifu kona ya Juma Abdul kabla ya dakika ya 80 mchezaji wa zamani wa Mbao FC kumtilia pasi nzuri Akilimali aliyepiga shuti lililotua mikononi mwa kipa wa Polisi, Kondo Salum.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Beno Kakolanya/Youthe Rostand dk46, Juma Abdul, Hassan Kessy/Burhan Akilimali dk46, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani/Said Juma ‘Makapu’ dk50, Pius Buswita, Maka Edward/Papy Kabamba Tshishimbi dk46, Amissi Tambwe, Yussuf Mhilu/Geoffrey Mwashiuya dk46 na Emmanuel Martin/Yohanna Nkomola dk74.
  Polisi Tanzania; Kondo Salum/Ally Abdul dk84, James Ambrose, Juma Ramadhan, Lakini Mwakalukwa, Ezekiel Lawi, Abdallah Mudhihiri, Benedicto Elius/Ahmad Kambangwa dk49, Jeremiah Katula, Jackson Wawa, Tizzo Chomba na Ally Mabuya.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WASHINDWA KUFURUKUTA KWA POLISI TZ, SARE 0-0 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top